WASICHANA WATATU MBARONI KWA KUCHAFUA PICHA YA RAIS NKURUNZIZA


Wasichana watatu wa shule nchini Burundi wanashikiliwa mahabusu kwa kuchafua picha ya rais Pierre Nkurunziza.

Wasichana hao wenye umri wa miaka 15, 16,na 17 wanaosoma shule moja ya sekondari darasa la saba kaskazini mwa Burundi, wamekuwa kizuizini kwa siku kumi zilizopita walipatikana na hatia ya picha ya rais pierre Nkurunziza wa Burundi iliyo kwenye vitabu vyao vya shule.

Walikamatwa walipokuwa katika shule ya ECOFO iliyopo katika mkoa wa kaskazini wa Burundi wa Kirundo tarehe 12 mwezi huu wa Machi,2019.

Awali walishitakiwa wakiwa wanafunzi saba, lakini wanne wakaachiliwa huru.

Watatu hao wanashikiliwa kwenye gereza la wanawake la mkoa wa Ngozi.

Mashirika ya haki za watoto yanaomba watoto hao waachiwe huru na kesi wakati kesi ikiendelea.

Makundi ya haki za binadamu yalituma vibonzo vinavyoonyesha picha ya Nkurunziza iliyochafuliwa kwa michoro kwenye kurasa za mtandao wa twitter, kuonyesha kuwa wanapinga kukamatwa kwa watoto hao wa shule.
Shirika la kutetea haki za watoto nchini humo limesema liliwatafutia wakili ambaye anafuatilia keshi yao.

''Wakili wa watoto hao anafuatilia kwa karibu kesi hiyo, na sisi kwenye muungano wetu wa kutetea haki za watoto tunafuatilia kwa karibu sana. Tayari tumetoa tumeomba watoto hao waachiliwe huru wakati uchunguzi wa kesi ukiendelea. Hakuna ushahidi kwamba hakika ni watoto hao waliokamatwa miongoni mwa wengine wengi ndiyo walio husika na na pia mtoto atapo fungwa siku nyingi na baadae kukutwa hana hatia inaweza muachia madhara makubwa''. Amesema mkuu wa shirika hilo, Ferdinand Simbaruhije.

Katika mahojiano na BBC na wakili wa wasichana hao Francois Kayonde aliyeko mjini Kirundo kaskazini mwa Burundi nyumbani kwao watuhumiwa amesema: Wateja wake watoto wa shule wamejitetea kwamba ,vitabu hivyo si vipya,na pia wanabadilishana vitabu hivyo siyo kwamba kila mmoja ana kitabu chake.

Wakili francois Kayonde anasema angependelea kesi ianzishwe haraka.

Mwandishi wa BBC mjini Bujumbura anasema Tukio kama hili la wanafunzi kushutumiwa kuharibu picha ya rais wa Burundi si geni.

Mnamo mwaka 2016 shule mbali mbali mjini Bujumbura na mikoani watoto kadhaa walitiwa mbaroni wakihusishwa na matukio ya aina hiyo.

Shirika la kutetea watoto FENADEB lilikua msitari wa mbele kuwatetea watoto hao.

Mashirika ya kutetea haki za watoto nchini Burundi yameshauri uchunguzi wa kina ufanyikekabla ya kuwatia watoto hao hatiani ili kubaini ni kwa nini matukio kama hayo yanajitokeza.

Ikiwa ombi la kuwaachilia huru wanafunzi hao watatu litakubalika ama kutokubalika ni jambo la kusubiri, lakini kwa sasa wasichana 3 watabaki kizuwizini hadi siku thelathini, kulingana na sheria na uamuzi wa mahakama.

Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post