MVUA KUBWA YAZUA KIZAA ZAA DAR

Mvua kubwa imenyesha jiji Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Jumapili na bado inaendelea “kupiga” katika maeneo kadhaa jijini Dar es salaam. 

Taarifa kutoka maeneo mbalimbali za jiji hili zinasema, mvua nyingi imenyesha katika maeneo ya Kariakoo, Jangwani, Ilala, Kinondoni Bunju hadi Bagamoyo.

“Ukanda wote huu wa Pwani, mvua kubwa imenyesha na kwa mujibu wa taarifa ya hali hewa, mvua hizo zitaendelea kunyesha hadi Mei mwaka huu,” ameeleza mtaalam mmoja kutoka Idara ya hali hewa.

Mtaalam huyo ambaye hakupenda kutajwa jina kwa kuwa siyo msemaji wa Idara hiyo anasema, “utabiri unaonyesha kuna mvua kubwa zinazoweza kunyesha na huenda zikaleta maafa.”

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia magari kadha yakiwa yamekwama kwenye maji maeneo ya Kariakoo na Jangwani.

“Hapa Jangwani, kote kumejaa maji. Katika eneo la magari ya Mwendokasi, maji yamejaa na kuathiri kwa kiwango kikubwa usafiri,” ameeleza mmoja wa mashuhuda.

Katika eneo la Kariakoo, hasa barabara ya Nyerere aneo la Gerezani, magari kadhaa yalikwama na mengine kuzimika.

Kufuatia hali hiyo, baadhi ya vijana wanaofanya biashara ndogo ndogo katika maeneo hayo, walitumia fursa ya mkwamo; na au kuzimika wa magari hayo, kujipatia ajira.

Wengi wao walijitosa barabarani na kuanza kusaidia kukwamua baadhi ya magari yaliyokwama.

Kioja kikubwa kilikuwa pale gari la wagonjwa – Ambulance – lilizimika.

Baadhi ya vijana waliombwa kusaidia kulikwamua gari hilo, walilikwepa kwa hoja kuwa “mgonjwa hana hela.”

Chanzo - Mwanahalisionline

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527