MEYA WA MANISPAA YA MTWARA ATIMKIA CCM

Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani ambaye pia ni Diwani wa kata ya Tandika, Geoffrey Isack Mwachisye ametangaza rasmi kujiunga na chama cha Mapinduzi(CCM) akitokea Chama cha wananchi (CUF).

Mwanchisye ametangaza uamuzi huo hii leo Machi 27, 2019 kwenye ofisi za Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mtwara, mbele ya Katibu wa CCM Mkoa El-Haj Kusilawi na viongozi wengine wa chama cha mapinduzi wilaya.

"Kimsingi nimeamua kuungana na chama cha mapinduzi ili kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna ambaye ametutishia wala kutupa fedha", amesema Mwanchisye.

"Mimi kama Meya nilikua napambana kutekeleza majukumu lakini 'Combination' ya timu niliyotoka haikua nzuri, tumeona kuna kila haja ya kurudi kwa kocha mahiri ambaye ni Rais Magufuli, nitakuwa muaminifu wa chama na kwa nchi yangu".

Aidha Meya Mwanchisye ameambatana na diwani wa Kata ya Chikongola (CUF), Musa Namtema (Fasheni) ambaye naye amejiunga na CCM huku akitoa sababu ya kwamba anaamini CCM ni chama ambacho kitawawezesha kuwatumikia wananchi vizuri kwa kutekeleza ilani ya chama kilicho madarakani.

Kabla ya kutimkia CCM Meya Mwanchisye amewahi kutajwa kutofautiana na viongozi waandamizi wa Chama chake cha awali (CUF), ngazi ya wilaya, baada ya kusimamia upitishwaji wa sheria ndogo ya ongezeko la Kodi ya mabanda ya biashara kulikopelekea wafanyabiashara mjini Mtwara kugoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527