Picha : RC SHINYANGA ATAMBULISHA MRADI WA 'BADILISHA TABIA TOKOMEZA MALARIA' UNAOTEKELEZWA NA T-MARCMkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack ametambulisha rasmi mradi wa 'Badilisha Tabia Tokomeza Malaria' unaotekelezwa na asasi ya T- MARC Tanzania kwa ajili ya kazi za uhamasishaji jamii kupambana na ugonjwa wa malaria katika halmashauri za wilaya za Ushetu,Msalala na Kishapu  mkoani Shinyanga.Mradi huo umetambulishwa leo Jumanne Machi 5,2019 katika ukumbi wa Submarine Hoteli Mjini Kahama wakati wa mkutano wa utambulisho wa mradi huo uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa kutokomeza Malaria.Lengo la mradi huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili ni uhamasishaji wa kuzuia ugonjwa wa malaria ambapo walengwa ni akina mama wajawazito,wanaonyonyesha,walezi wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na watoa huduma kwenye kliniki za akina mama na watoto.Akitambulisha mradi huo,Telack alisema ripoti ya Viashiria vya maambukizi ya Malaria ngazi ya jamii ya mwaka 2017/2018 inaonesha kuwa maambukizi ya ugonjwa wa malaria yamefikia asilimia 6 kutoka asilimia 17 kwa mwaka 2015/2016.

“Pamoja na kupungua kwa maambukizi kulikochangiwa na juhudi za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa mikakati ya udhibiti wa malaria iliyopo inatakelezwa kwa ufanisi,hivyo bado juhudi zinatakiwa kufanyika ili kupunguza kiwango hiki kufikia asilimia 1 na hatimaye kutokomeza kabisa Malaria katika mkoa wetu”,alieleza.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015-2020) wa Kudhibiti Malaria ulioandaliwa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, kumekuwepo mafanikio mkoani Shinyanga ikiwemo kuongezeka kwa uwepo wa vyandarua vyenye dawa kwa jamii.

Aidha alisema kutokana na kuwepo kwa mwitikio mdogo wa wanajamii kushiriki katika mikakati ya kupambana na malaria ni imani yake kwamba kupitia mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria utatumika kuhamasisha jamii kushiriki kwenye mikakati ya kudhibiti malaria kwa vitendo.

Telack aliwataka viongozi na wataalamu wa ngazi ya mkoa,wilaya na halmashauri kushirikiana na T- MARC kutekeleza mradi huo vizuri ili kutokomeza Malaria huku akiitaka T-MARC kujipanga kutekeleza mradi huo kwenye mkoa mzima.

“Malaria inazuilika na inatibika,tiba ya mapema baada tu ya dalili za homa kuanza ni muhimu kuzuia vifo hususani kwa watoto na akina mama wajawazito”,aliongeza Telack.

Awali Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy alisema kupitia mradi watahamasisha wanawake wajawazito,wanaonyonyesha na watoto kutumia vyandarua vyenye dawa kuzuia ugonjwa wa malaria lakini pia jamii kupima afya badala ya kuanza kutumia dawa kwani siyo kila homa ni malaria.

Naye Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima aliwataka wananchi kuondokana na dhana potofu kuwa vyandarua vinapunguza nguvu za kiume huku akiwahamasisha kutumia vyandarua kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria' unatekelezwa na asasi ya T- MARC Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  ili kutekeleza Mpango Mkakati  wa Taifa wa Kudhibiti Malaria.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akizungumza wakati wa kutambulisha mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria unaotekelezwa na asasi ya T- MARC kwa ajili ya kuhamasisha jamii kupambana na ugonjwa wa malaria katika halmashauri za wilaya za Ushetu,Msalala na Kishapu  mkoani Shinyanga - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack, akiwasihi viongozi na wataalamu kushirikiana na asasi ya T- Marc kutekeleza mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria.Wa kwanza kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Mohammed Kahundi akifuatiwa na Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima. Wa kwanza kushoto ni Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akielezea kuhusu hali ya viashiria vya maambukizi ya Malaria mkoani Shinyanga.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akiwahamasisha viongozi na watalaamu wa afya kwa kushirikiana na wadau kuongeza jitihada katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria ambao umekuwa ukichangia vifo vya mama na watoto.
Kushoto ni Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- Marc, Hamid Al- Alawy akifuatiwa na Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka T- MARC, Levina Thobias na Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima (kulia).
Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima akielezea kuhusu Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015-2020) wa kudhibiti Malaria ulioandaliwa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto.
Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima akiwasilisha mada ukumbini.
Wadau wakiwa ukumbini.
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- Marc, Hamid Al- Alawy akielezea kuhusu mradi huo na shughuli mbalimbali zinazofanywa na T-MARC katika kuwahudumia wananchi.
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akiwasilisha mada kuhusu asasi ya T- MARC.
Wadau wa kupambana na ugonjwa wa malaria wakiandika dondoo muhimu.
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akionesha kiwango cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kwa kipindi cha miezi 24.
Wadau wa kuzuia ugonjwa wa malaria wakiwa ukumbini.
Wadau wakiwa ukumbini.
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka T- MARC, Levina Thobias akiwasilisha mada kuhusu tafiti mbalimbali zilizofanywa na T-Marc ambapo walibaini kuwa bado jamii ina imani potofu kuwa utumiaji wa vyandarua unapunguza nguvu za kiume lakini pia kuleta kunguni.
Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha akiwataka wadau wanaotekeleza miradi mbalimbali wilayani Kahama kuhakikisha wanatumia lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza akibainisha kuwa baadhi ya wadau wamekuwa wakisambaza vipeperushi vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza wakati wananchi wanaelewa vizuri zaidi Kiswahili. 
Wadau wakifuatilia matukio yaliyokuwa yanaendelea ukumbini.
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akiwaomba viongozi na wataalam mbalimbali kushirikiana na T-Marc ili kufanikisha mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria.
Kaimu Mganga Mkuu mkoa wa Shinyanga, Dkt. Nuru Mpuya akitoa neno la shukrani baada ya Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutambulishwa na kuahidi kushirikiana na T-MARC kutekeleza mradi huo.
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akiagana na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack.
Picha ya pamoja : Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack, viongozi,wataalamu na wadau wa kupambana na malaria.
Picha ya pamoja.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post