ZITTO KABWE APOKELEWA KWA SHANGWE ZANZIBAR

Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe leo amewasili visiwani Zanzibar na kupokelea na mamia ya wanachama hicho akiwamo Maalim Seif Sharif Hamad.


Zitto amewasili katika ofisi mpya za ACT- Wazalendo zilizopo Vuga, Unguja ambazo awali zilikuwa makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) visiwani humo.

Baada ya kuwasili katika ofisi hizo saa 4.36 asubuhi, Maalim Seif alimpokea Zitto huku mamia ya wana ACT- Wazalendo wakimpokea kwa nyimbo mbalimbali.

Zitto na Maalim walivalishwa mataji kisha wakaenda kukaa eneo maalum lililoandaliwa.

Alipopewa fursa ya kusalimia, Zitto amesema, “Nina furaha sana leo, nataka kuwahakikishia tumeshashusha tanga, tumeshapandisha tanga, safari inaendelea.”

Maalim Seif amewasalimia wafuasi wa chama hicho akisema: “ACT-Wazalendo”.

Ilipofika saa 4.52 asubuhi, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini na Maalim Seif aliyewahi kuwa katibu mkuu wa CUF pamoja na baadhi ya viongozi waliingia ndani huku nyimbo zikiendelea kutumbuiza na wanachama wakicheza.

Maalim Seif pamoja na viongozi mbalimbali waliokuwa CUF Machi 18 walikabidhiwa kadi za uanachama wa ACT- Wazalendo katika shughuli iliyofanyikia makao makuu ya ACT- Wazalendo, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Na Haji Mtumwa, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post