LIPUMBA ACHAGULIWA TENA KUWA MWENYEKITI WA CUF...NAFASI YA MAALIM SEIF YAWEKWA KIPORO

Mkutano mkuu wa CUF umemchagua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyeki wa chama hicho, huku nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ikiwekwa kiporo.

Maalim Seif, katibu mkuu wa chama hicho amewekwa kiporo kutokana na mabadiliko ya katiba yaliyofanyika juzi ambayo yamempa nguvu mwenyekiti kuteua majina matatu ya wanachama kwa kushauriana na makamu wenyeviti wa Bara na Zanzibar.

Baada ya hatua hiyo, majina hayo yatapelekwa katika kikao cha Baraza la Uongozi ambalo litakuwa na jukumu la kumpigia kura mmoja.

Mabadiliko hayo yaliyofanywa na mkutano huo yamefuta utaratibu wa awali ambao katibu mkuu alikuwa akichaguliwa na mkutano mkuu na sasa Profesa Lipumba atakuwa ameshikilia hatima ya Maalim Seif.

Uchaguzi huo umefanyika kipindi ambacho CUF iko katika mgogoro mkubwa wa kiuongozi ulioigawa katika pande mbili - mmoja ukiwa wa Profesa Lipumba na ule wa Maalim Seif.

Mgogoro huo umekifikisha chama hicho mahakamani ambako kuna kesi kadhaa ikiwamo ya kumpinga Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti na Machi 17, hukumu ya ama ni mwenyekiti au la itatolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika mkutano huo ulioanza juzi ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliubariki kwa kuufungua kupitia naibu msajili wa vyama, Sisty Nyahoza, hatimaye jana ulimchangua Profesa Lipumba.

Baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza, Profesa Lipumba alisema jambo la kwanza wanalokwenda kufanya ni kutibu majeraha yaliyotokana na mgogoro uliopo ndani ya chama hicho. “Atakayeendeleza migogoro iliyopita wakati tunatibu majeraha hatua kali zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.

Na  Kalunde Jamal na Hellen Hartley Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527