KIGOMA WAZINDUA SANAMU YA 'SAMAKI MGEBUKA" ...RC MAGANGA AONYA WIZI WA MIUNDO MBINU

Muonekano wa Mnara wa Mgebuka mkoani Kigoma

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga amewataka vijana mkoni Kigoma  kuacha wizi wa miundombinu ya serikali  na kwa atayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


Mkuu huyo wa mkoa amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Sanamu ya Samaki aina ya Mgebuka ambapo amesema kumekuwa na tabia ya vijana wengi kuiba taa za barabarani  na wengine kuvamia majumbani na kuiba, na kuwataka waache tabia hiyo na kufanya kazi.

Aidha aliagiza kuanzia sasa wafanyabiashara mkoani humo waanze kufanya kazi hadi saa sita usiku tofauti na mwanzo ambapo walikuwa wakifunga maduka yao saa kumi na mbili jioni kwa kuwa  sasa ulinzi umeboreshwa mkoani na miundombinu imeboresha kwa kuwa serikali imejipanga kuwasaidia wananchi kuleta maendeleo.

Alisema kwa yeyote atakayekamatwa akijihusisha na ujambazi hawatamvumilia huku akitoa onyo kwa kikundi cha vijana kinacho jihusisha na masuala ya ubakaji na wizi kuacha mara moja na endapo watakamatwa serikali itawachukulia hatua.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa barabara TANROADS Naris Choma alisema ujenzi wa  sanamu ya Samaki  ni maagizo ya Serikali  kwamba barabara zote zinazohudumiwa na TANROADS  kuboreshwa ili ziweze kuwa na maandhari nzuri na ziweze kuwahudumia wananchi na leo wameanza na sanamu ya Mgebuka inaashiria ni samaki anayepatikana katika Ziwa Tanganyika na kwa heshima ya Wakazi wa Kigoma kuweka Sanamu hiyo kuonyesha vivutio vilivyopo mkoani Kigoma.

 Alisema ujenzi wa sanamu umegharimu kiasi cha shilingi milioni saba na laki moja na umeambatana na uzio ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 187 pamoja na taa.

Alisema pia wanatarajia kufanya upanuzi wa mifereji na upanuzi wa barabara, ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu katika soko la Kigoma kupunguza msongamano wa watu na magari.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Alex Dackriss waliipongeza serikali kwa  kujenga sanamu hiyo kwa kuwa walizoea kuona samaki Mwanza na wanaahidi kuitunza miundo mbinu hiyo kwa kuwafichua  wote watakaobainika kufanya wizi wa miundombinu ya serikali.

Naye Juma Kizza aliishukuru serikali kuruhusu biashara kufanyika hadi saa sita usiku na kuomba ulinzi  kuimarishwa  na kuboresha miundombinu itakayoruhusu  biashara kufanyika.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga akikata utepe wakati  wa uzinduzi wa Sanamu ya Samaki aina ya Mgebuka. Picha zote na  Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Muonekano wa  Sanamu ya Samaki aina ya Mgebuka 
Wakazi wa Kigoma wakifurahia na migebuka yao

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527