WAZIRI MKUU AFUNGA SOKO KIGOMA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza kufungwa kwa soko la wakimbizi na wananchi lililoanzishwa nje ya kambi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma.

Hatua hiyo imekuja baada ya soko hilo kubainika kuwa chanzo cha wakimbizi kutoka nje ya kambi kiholela na kushiriki katika kufanya matukio ya kiharifu.

Ametangaza uamuzi huo leo (Jumanne, Februari 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa umma katika Halmashauri ya Kibondo ambapo amesema, "vitendo vya uhalifu wilayani Kibondo vikiwemo vya utekaji wa watoto vimeongezeka na kusababisha hofu na taharuki miongoni mwa wananchi.”

Waziri Mkuu amesema ni vema halmashauri hiyo ikaandaa utaratibu wa kutoa vibali vitakavyowaruhusu Watanzania kupeleka bidhaa ndani ya kambi hivyo.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wananchi waliopewa dhamana ya kufanya kazi kwenye kambi za wakimbizi wawe waadilifu na wasimamie sheria.

“Nafahamu tunao watendaji wetu ambao wapo kambini kusimamia shughuli mbalimbali za wakimbizi, tekelezeni wajibu wenu ipasavyo na si vinginevyo.”

Baada ya kuzungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Kibondo, Waziri Mkuu alikwenda wilayani Kakonko na kukagua mradi wa maji Muhange.

Pia Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Kakonko unaotarajiwa kugharimu sh. bilioni 4.5.

Chanzo - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527