Picha : SHIRECU YAANZA KWA KASI UJENZI WA UZIO SHULE YA SEKONDARI BULUBA



Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) mkoani Shinyanga, kimeanza kujenga uzio wa Shule ya Sekondari Buluba ambayo ni moja ya miradi inayomiliki kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama kwa wanafunzi pamoja na miundombinu ya Shule hiyo.



Akizungumza  leo Februari 19, 2019 wakati akikagua uchimbaji wa msingi na ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya kujenga uzio wa shule hiyo,Makamu Mwenyekiti wa SHIRECU, Enock Lyeta amesema ujenzi huo utakamilika mwezi Agosti,2019.

Amesema shule hiyo ilijengwa mwaka 1967 na kwa miaka mingi imekuwa haina uzio jambo ambalo limekuwa likihatarisha usalama wa maisha ya wanafunzi pamoja na uharibifu wa miundombinu kutokana na vibaka kuvamia shuleni hapo mara kwa mara.

“Tarehe 25.10.2018 wakati tukiadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya shule ya Buluba tukiwa na mgeni rasmi aliyekuwa Waziri wa Kilimo Charles Tizeba, tuliendesha harambee ya ujenzi wa uzio wa shule hii, na kufanikiwa kupata shilingi milioni 64 na mifuko ya saruji 1,300, ambapo ujenzi wake ndiyo tumeuanza sasa na utakamilika Agosti mwaka huu,”amesema Lyeta.

“Mbali na ujenzi wa uzio huu pia sehemu zingine tutajenga maduka ambayo yatazunguka shule, na ujenzi wa mabweni, ili kuiboresha shule kuwa katika mazingira mazuri kama zamani,”ameongeza.

Naye mkuu wa shule hiyo Frednand Chuwa amepongeza ujenzi wa uzio shuleni hapo  ambapo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uvamizi wa vibaka na kupora vitu vya wanafunzi wa bweni pamoja na kuharibu miundombinu ya shule hiyo.

Amesema mbali na uvamizi huo wa vibaka pia wanafunzi wa kike wamekuwa na tabia ya kutoroka majira ya usiku, na kwenda kwenye sehemu za starehe ikiwemo disko lakini uzio huo utakapokamilika kujengwa utasaidia kuondoa changamoto hizo shuleni hapo.

Nao baadhi ya wanafunzi shuleni hapo akiwemo James Paulo na Grace Swalehe, kwa nyakati tofauti wamekiri kuwepo na changamoto hizo shuleni hapo na kubainisha kuwa ujenzi wa uzio huo utasaidia hata kupunguza kasi ya wanafunzi kutoroka mara kwa mara na hatimaye kuongeza ufaulu.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Makamu Mwenyekiti wa SHIRECU  Enock Lyeta ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Buluba (Mwenye suti ya bluu), akiwa na mkuu wa shule hiyo ya Buluba Frednand Chuwa (kulia) wakikagua ufyatuaji wa matofali ambayo yatatumika kwenye ujenzi wa uzio wa shule hiyo. Na Marco Maduhu - Malunde1 Blog

Makamu mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) Enock Lyeta ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Buluba (Mwenye suti ya bluu), akiwa na mkuu wa shule hiyo ya Buluba Frednand Chuwa, wakikagua matofali ambayo yameshafyatuliwa kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule hiyo.

Ukaguzi wa matofali ukiendelea. Kushoto ni Mtaalamu wa IT kutoka SHIRECU, Dotto Joshua.

Muonekano wa matofali ambayo yameshafyatuliwa kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika shule ya Sekondari Buluba mjini Shinyanga.

Muonekano wa matofali ambayo yamesha fyatuliwa kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika shule ya Sekondari Buluba mjini Shinyanga.

Mafundi wakiendelea na kazi ya kufyatua matofali ambayo yatatumika kujenga uzio wa shule ya sekondari Buluba ambayo inamilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) Mkoani Shinyanga.

Makamu mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) Enock Lyeta (Mwenye suti ya Blue) akikagua uchimbaji wa Msingi wa uzio katika shule ya Sekondari Buluba iliyopo mjini Shinyanga.

Ukaguzi wa uchimbaji wa msingi ukiendelea katika uzio wa shule ya Sekondari Buluba.

Makamu mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) Enock Lyeta ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya Shule ya Sekondari Buluba, akielezea namna wanavyojikita kuimarisha miundombu ya shule hiyo kwa kuanza na ujenzi wa uzio, mabweni pamoja na maduka ili kuongeza kipato cha Shule.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Buluba Frednand Chuwa, akielezea umuhimu wa uzio kwenye shule hiyo kuwa itapunguza utoro kwa wanafunzi, kuimarisha ulinzi na usalama kwa wanafunzi pamoja na miundombinu ya shule hiyo na kutoa wito kwa wazazi kupeleka wanafunzi shuleni hapo ikiwa wameshaongeza kozi zingine za PCM, EGM,HGE pamoja na KLF.

Mwanafunzi James Paulo anayesoma Kidato cha Sita katika shule ya Sekondari Buluba HKL, amepongeza ujenzi wa uzio huo ambao utasaidia pia kupunguza kelele za magari na kuwatoa kwenye umakini wa usomaji, pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama kwao.

Matha Charles ambaye anasoma katika shule ya sekondari Buluba kidato cha Nne, anasema ujenzi wa uzio huo utasaidia pia kuondoa changamoto ya kuvamiwa na vibaka shuleni hapo hasa kwa wanafunzi ambao wanaishi bweni pamoja na kutoroka kwenda kwenye disko usiku.

Na Marco Maduhu - Malunde1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527