SIMBA YAENDELEZA UBABE... YAICHAPA AZAM FC 3 - 1


 Timu ya Simba imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuifunga Azam FC mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa leo Ijumaa.

Bao la mapema dakika ya 4 lililofungwa na Meddie Kagere liliwainua mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo.

Kagere ndiye alikuwa wa kwanza kupachika bao dakika tano akifunga kwa kichwa kumalizia mpira uliopigwa na Bocco na kumwacha kipa wa Azam FC Razak Abarola akishangaa.

Vijana hao wa Msimbazi waliongeza bao la pili dakika ya 38, kupitia kwa Nahodha John Bocco 'Adebayor' ambaye pia alifunga kwa kichwa kutokana na krosi ya Zana Coulibaly na kuifanya Simba iende mapumziko ikitamba kwa kipindi hicho.

Kagere aliweka wavuni bao la tatu dakika ya 77 huku akishangilia kwa namna yake kwa kutafuta mpira baada ya kuingia nyavuni.

Azam FC walipata bao la kufutia machozi dakika ya 81’ likiwekwa wavuni na Frank Domayo.

MCHEZO ULIVYOKUWA...

 Ikitumia mfumo wa 4:3:3 Simba walionyesha uimara katika safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na Kagere, Bocco na Emmanuel Okwi katika kutafuta mabao kwa ushirikiano.

Lakini pia safu ya ulinzi chini katikati iliyokuwa na Pascal Wawa na Paul Bukabana ilikuwa imara kuzima mashambulizi ya Azam FC ambao iliwabidi washambuliaji wao Ramadhan Singano, Obrey Chirwa na Tafadzwa Kutinyu kupiga mashuti ya mbali.

Dakika ya 14, Simba walifanya mashambulizi kupitia kwa Kagere lakini shuti lake lilitoka nje.

Chirwa alipambana akapata nafasi dakika ya 24 lakini akapaisha mpira ukatoka nje. Kiungo Salum Aboubakary 'Sure Boy' ambaye alionyesha inshore kwenye safu hiyo kwa kukaba na kushambulia alipiga shuti kali dakika 33, lakini liligonga mwamba na kutoka nje.

Azam FC pia walitumia mfumo wa 4:3:3 walifanya mashambulizi mengi kupitia pembeni kama ambavyo Simba walifanya.

Na Doris Maliyaga - Mwanaspoti

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post