SIMAI : TAMASHA LA SAUTI ZA BUSARA NI LA WAZANZIBAR WOTE


Mwakilishi wa Balozi wa Norway nchini na Mkuu wa Idara ya Ushirikiano, Trygve Bendiksby akizungumza katika tukio na waandishi wa habari leo kwa waandishi wa habari mjini Unguja, Zanzibar. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Busara Promotions, Simai Mohammed Said, akifuatiwa na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Bi. Tinguely Mattli mwishoni kulia ni Mkurugenzi wa Busara Promotions, Mahmoud Yusuf, kushoto ni Meneja wa tamasha hilo, Ramadhani Journey leo Februari 7, 2019.(Picha zote na Andrew Chale)
Kikundi cha Mwiduka kutoka Mkoani Mbeya kikitoa burudani katika tukio hilo la mkutano wa utambulisho kwa vyombo vya Habari, Zanzibar.

Kikundi cha Mwiduka kutoka Mkoani Mbeya kikitoa burudani katika tukio hilo la mkutano wa utambulisho kwa vyombo vya Habari, Zanzibar.


Na Andrew Chale - Zanzibar 

Wafanyabiashara na wananchi wote wa Zanzibar, wametakiwa kuwa kifua mbele kila msimu wa uwepo wa tamasha kubwa la Kimataifa la muziki la Sauti za Busara kwa kuwa tamasha hilo linabeba taswira chanya ya maendeleo ya Wanzibar wote.

Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari, Zanzibar, Mwenyekiti wa Bodi ya Busara Promotions, Simai Mohammed Said, amesema tamasha hilo la siku nne ni kichocheo cha uchumi kwani watu wanafika mbali na kulishuhudia lakini pia wanafanya manunuzi na matumizi ndani ya Visiwa hivyo na kuongeza pato la serikali.

Amewataka kuchangamkia fursa ya uwepo wake kila mwaka kwani limekuwa likileta wageni wengi wanaokuja nchini kuhudhuria tukio hilo kubwa lenye kuvutia watu mbalimbali duniani kote.
“Kuanzia leo tutashudia burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali wa ndani na nje, wanamuziki hao wataonesha nyimbo za tamaduni za nchi zao huku pamoja na kutoa burudani na mafunzo kwa watu wote.

Muziki ni biashara, muziki ni kazi na ni kazi kubwa hivyo ili kuwaunga mkono wasanii hawa ni kujitokeza kushuhudia tamasha hili ambapo pia tumetoa ofa ya punguzo kubwa kwa wenyeji.” alisema Simai.

Aidha, Simai alisema viongozi wa Busara Promotions ambao ni waasisi na waandaaji wa tamasha hilo, wamekuwa wakifanya kila aina ya mbinu kuhakikisha linaandaliwa na kufanyika kwa ubora uliokusudiwa hivyo ni juu ya wananchi haswa wazanzibar kulikubali na kulithamini ili kuinua hadhi ya Zanzibar kimataifa.

“Ili tamasha ni la kwenu Wazanzibar. Tuliinue tulipendemilango ipo wazi kwa wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kulidhamini kwa aina yoyote ile ya udhamini utapokelewa. Tunahitaji liweze kuwa thamani zaidi na tulienzi kwa kiwango cha juu” alisema Simai ambapo amesisitiza kuwa uwepo wa tamasha hilo si kwa ajili ya kuvutia watalii pekee bali kwa watu wote kwenye nyanja za Utamaduni, mila na desturi za mwafrika kupitia njia ya muziki.

Simai pia amesisitiza kwa vyombo vya habari na wataalamu wa teknolojia ya habari Nchini kuendelea kuwaunga mkono katika kutangaza taarifa za habari za tamasha hilo ikiwemo mandhari ya mji wa Zanzibar ili lionekane duniani kote na kuwatia hamu wale ambao hawajawahi kufika Zanzibar kuamua kwenda kushuhudia.

Kwa upande wao Mabalozi wa Uswis na Norway wanaoziwakilisha nchini zao hapa Tanzania, wamewapongeza Busara Promotions kwa namna wanavyoendesha tamasha hilo ikiwemo kukuza tamaduni za Mwafrika kupitia njia za Sanaa.

Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Bi. Tinguely Mattli amesema wanaamini tamasha hilo ni moja ya njia ya kufikisha ujumbe kwa wananchi kupitia wasanii ambao wamekuwa ni kioo cha jamii.

Nae Mwakilishi wa Balozi wa Norway nchini na Mkuu wa Idara ya Ushirikiano, Trygve Bendiksby alisema kupitia kauli mbiu ya mapambano dhdi ya rushwa ujumbe utafika kwa wakati na haraka kupitia wasanii ambao jamii imekuwa ikiwafuatilia kwa ukaribu hivyo wataendelea kudhamini tamasha hilo kwa kipindi kingine.

“Tunaungana na Busara Promotions kwenye tamasha ili kubwa na tutaendelea kulidhamini tamasha kwa kipindi kipindi cha miaka mitatu mingine”, alisema Bendiksby.

Ubalozi huo wa Norway na Busara Promotions wanatarajia kutiliana saini ya udhamini wa miaka mitatu mingine hapo baadae. Tayari Norway imeweza kulidhamini tamasha hilo kwa muda wa miaka tisa (9) kwa kipindi tofautitofauti.

Naye Mkurugenzi wa Busara Promotions, Mahmoud Yusuf amesema kuwa, wamekuwa wakipokea maombi mengi ya wasanii ndani na nje ambapo walio na sifa ndio wenye kuchaguliwa kila mwaka ambapo kwa mwaka huu karibu wote waliochaguliwa ni wa kiwango cha juu.

“Watu ni wengi na karibu hoteli zote zenye hadhi ya nyota nne na tano hususan maeneo ya Mji Mkongwe zimejaa na maeneo mengine watu wamejiandaa kwa ajili ya tamasha ili kubwa visiwani hapa”, alisema Yusuf.

Yusuf alisema, wenyeji wamepewa nafasi ya kipekee ya kushuhudia tamasha hilo kwa bei ya ofa maalum kwa siku tsh. 10,000 huku kwa siku zote nne akitakiwa kulipa tsh. 20,000 huku akitaka pia wawe mfano wa kuigwa kwa kuonesha ukarimu na upendo kwa wageni kuanzia vyombo vya usafiri maeneo ya mitaa na manunuzi ili wajisikie wapo na wenyeji wenye moyo wa kupokea wageni.

Naye Meneja waTamasha hilo, Ramadhan Journey alisema kuwa, kwa mwaka huu ni la 16 vikundi 44, vinatarajia kuonesha burudani kwa siku nne kwenye majukwaa matatu tofauti ya katika ukumbi wa kihistoria wa ‘Old Fort’ mjini Stone Town, Zanzibar.

Aidha, Journey ametaja baadhi ya orodha ya Wasanii kwa mwaka huu ni akiwemo: Fid Q kutoka Tanzania Bara, Wasanii wengine na Nchi zao kwenye mabano ni pamoja na: Mokoomba (Zimbabwe), Afrigo Band (Uganda), Fadhilee Itulya (Kenya), Ifrikya Spirit (Algeria), Rajab Suleiman & Kithara ( Zanzibar), Tune Recreation Committee, (Afrika Kusini), Ithrene (Algeria). Hoba Hoba Spirit (Morocco).

Pia wamo: M'Toro Chamou (Mayotte/Reunion), Trio Kazanchis +2 (Ethiopia/Switzerland), Faith Mussa (Malawi), Shamsi Music (Kenya), Sofaz (Reunion), Dago Roots( Reunion), Lydol (Cameroun), Jackie Akello (Uganda), S Kide & Wakupeti Band (Tanzania), Tausi Women's Taarab (Zanzibar), Mkubwa na Wanawe Crew (Tanzania), Damian Soul (Tanzania) na Wamwiduka Band (Tanzania) na wengineo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527