POLISI 'WAMCHOMOA' MKURUGENZI WA HALMASHAURI MAUAJI KANISANI...WAUMINI WASISITIZA NDIYE ALIYEFYATUA RISASI


Unaweza kusema Jeshi la Polisi mkoani Singida ‘limemchomoa’ mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Pius Luhende katika tuhuma za kuhusika na mauaji ya Isaka Petro (28).

Taarifa ya polisi mkoani humo inaeleza kuwa watu saba wanashikiliwa akiwemo mkurugenzi huyo .

Taarifa hiyo ya Polisi inasema kuwa Luhende alipoingia ndani ya kanisa hilo ilitokea vurugu na akaamua kutoka nje kabla ya askari wanyamapori waliokuwa na silaha kufyatua risasi kadhaa na moja ikampiga Isaka na kufariki papo hapo.

Hata hivyo waumini waliokuwepo katika kanisa la Wasabato kijiji cha Kazikazi mkoani humo wakati mauaji hayo yakitokea Jumamosi iliyopita walipingana na polisi na kusema kuwa mkurugenzi huyo ndiye alimfyatulia risasi Isaka.

Alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweebert Njewike alishindwa kuikataa wala kuikubali taarifa hiyo, “kuhusu tukio hilo nimeshatoa taarifa tangu jana (juzi), hilo jambo nimeshalizungumza na kwa sasa nipo mpirani (Singida vs Yanga) nipigie baadaye.”

Mwananchi lilipotaka kufahamu zaidi kuhusu taarifa hiyo, hasa inavyoeleza kuwa mkurugenzi hakuwepo ndani ya kanisa alisema, “taarifa hiyo nimeshatoa.”

Taarifa hiyo imewataja watu wengine sita wanaoshikiliwa akiwemo mkurugenzi huyo kuwa ni Silvanus Lungwisha (ofisa kilimo na mifugo wa Itigi), Elik Paul (ofisa sheria Itigi), Eliutha Augustino (ofisa tarafa), Yusuph John (ofisa mtendaji wa kijiji cha Kazikazi), Rodey Elias na Makoye Steveni (wote maofisa wanyamapori).

Inaeleza kuwa mauaji hayo yalitokea baada ya Luhende kuwafuata watuhumiwa wa kosa la kuharibu mali na mlalamikaji Rose Andrew aliyedai kuharibiwa mali yake iliyopo ndani ya shamba la Tanganyika Packers linalomilikiwa na halmashauri hiyo.

“Maofisa walipata taarifa kuwa baadhi ya watuhumiwa wa kosa la kuharibu mali wapo katika Kanisa la Wasabato lililopo kijijini hapo ndipo walipokwenda kwa lengo la kuwakamata,” inaeleza taarifa hiyo.

Baba asimulia kifo cha mwanaye

Baba mzazi wa Isaka, Petro Chambalo alisema alikuwa na ugomvi na Luhende na kuna kesi mbili mahakamani alizodai kubambikiwa na mkurugenzi huyo.

Alisema tangu 2017 amekuwa akitofautiana naye na mara kadhaa ameagiza akamatwe na hakuna aliloelezwa zaidi ya kushinda siku nzima polisi na wakati mwingine kufikishwa mahakamani bila kusomewa shtaka lolote.

“Luhende ndiye alikuja na wenzake sita, alianza kuingia yeye na kufuatiwa na mtendaji wa kijiji kuanza kutupiga ngwala, lakini yeye ndiye alinyoosha bunduki kumpiga mwanangu,” alisema Petro.

Alisema mkurugenzi huyo aliingia kanisani akitaka John amuonyeshe aliokuwa anawataka huku nje risasi zikiwa zinapigwa.

“Waumini wengine walikuwa kimya na Isaka alisimama kuhoji mbona wamevamia kanisani kuna nini. Hakujibiwa zaidi ya mwenzetu James Jackson kuburuzwa nje akiwa amekabwa na watu wawili na mmoja nilimtambua ni ofisa kilimo anaitwa Lungwisha,” alisema.

“Nilisimama na kwenda kumsaidia nikitaka watuambie nini kimetokea, lakini mkurugenzi aliponishika nilimsukuma na hapo ndipo aliondoka kwenda kwenye gari yake kisha akachukua silaha na kurudi tena.”

Alisema wakati mkurugenzi akirejea tena kanisani, marehemu alikuwa akiimba nyimbo za sifa, “alizunguka upande wa dirishani watu wakimuona kisha akamlenga na kumpiga kichwani.”

Elias ambaye ni kaka wa marehemu alisema, “Alitoka (Isaka) mbele ya kanisa na kumsihi baba asigombane nao ndani ya kanisa. Alimsikiliza na kuacha lakini milango ikafungwa wakati risasi zikilia nje.”

“Mlango tulisaidia wote kuusukuma ukafunguka kisha tukajibanza kwenye kona wote wawili, lakini (huku akilia) niliona mtu anadondoka kugeuka nikakanyaga ubongo wake kwani kichwa kilifumuliwa.”

Alisema mkurugenzi huyo alikuwa na bunduki na walidhani kuwa atapiga risasi hewani lakini alimuelekezea mdogo wake na kufyatua risasi iliyopiga hadi ukutani.

Mke wa marehemu, Leah Pius alisema,”Mume wangu alikuwa anakaribia kupata daraja la uchungaji, ameniachia watoto watatu mkubwa akiwa na miaka sita tu.”

Kwa upande wake shuhuda mwingine wa tukio hilo, James alisimulia alivyobebwa juu kutolewa nje ya kanisa hilo, jinsi waumini wenzake walivyochukizwa na kitendo hicho na kuanza kuhoji kulikoni.

Neema Festo, mke wa mwinjilisti wa kanisa hilo, alisema wakiwa ndani ya kanisa aliingia mkurugenzi huyo na kutamka “Tumsifu Yesu Kristu”, akiwa ameongozana na mtendaji wa kijiji.

“Huyu Mtendaji wa Kijiji ndiyo namfahamu kabisa maana nyumba aliyopanga na nyumba ninayoishi zinatazamana hivyo namfahamu, aliingia na wengine pia wakawa wakali wakionyesha kama wanamtafuta mtu mwingine,” alisema.

“Lakini ujue pale paligeuka uwanja wa vita, hakuna mtu aliyetuambia tulale bali risasi zilikuwa zinapigwa nje mfululizo hadi nikahisi kama vile tuko vitani, mimi nilikuwa na wanangu hawa wawili nikaamua kujikunyata nao lakini nikiendelea kuimba mara nikasikia wameua ndo nikaona Shemasi amelala kichwa kimefumuliwa na ubongo kumwagika.”

Chanzo cha mgogoro

Mgogo wa ushuru wa mashamba katika mbuga ya kitongoji cha Boma la kati unatajwa kuwa ndiyo chanzo cha tukio kwani halmashauri inasema mashamba hayo ambayo awali yalikuwa yakimilikiwa na Tanganyika Packers ni sehemu yao.

Maswali 10

1. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi alifuata nini kanisani?

2. Je, ni kweli mkurugenzi huyo ana ugomvi na baba wa marehemu?

3. Je, mkurugenzi ndiye aliyetoa bunduki na kumfyatulia Isaka Isaka na kumuua?

4. Polisi wanasema tukio la mauaji lilitokea wakati mkurugenzi akiwa amekimbia je, ni nani aliyefanya mauaji hayo?

4. Polisi wanasema mkurugenzi huyo alikimbia na kufunga mlango, kwa nini alifunga mlango wa kanisa?

5. Baba wa marehemu anasema alishuhudia mkurugenzi akifyatua risasi, nani anazungumza ukweli, baba au polisi?

6. Je, ni kweli kuna kesi mbili mahakamani kati ya mkurugenzi na baba wa marehemu?

7. Kulikuwa na ulazima wowote wa mkurugenzi na msafara wake kwenda kudai ushuru wa mashamba kanisani?

8. Je, ni kawaida kwa mkurugenzi kupita mtaani kudai ushuru kwa wananchi?

9. Ni kwa nini Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo ameshiriki mazishi ya Isaka Isaka na kutoa ubani wa Sh1 milioni?

10. Je, ni kwa nini polisi, uongozi wa Singida haukutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kuzungumzia sakata hilo lilipotokea siku hiyo?
Na Habel Chidawali, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post