POLISI WASEMA MWANAHARAKATI CAROLINE AMEFARIKI AKITOA MIMBA YA MCHEPUKO

Polisi nchini Kenya wamesema kuwa uchunguzi wa awali uanaonesha kuwa kifo cha mwanaharakati maarufu Caroline Mwatha kimetokana na kutoa ujauzito wa miezi mitano.

Mara ya mwisho kwa mawanaharakati huyo kuonekana hai ilikuwa Jumatano ya wiki iliyopita kabla ya mwili wake kugunduliwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha City Mortuary mjini Nairobi.

Caroline Mwatha ni mwanaharakati aliyefanya kazi katika shirika la haki la kijamii katika kitongoji cha Dandora mjini Nairobi, shirika linalonakili visa vya mauaji ya kiholela yaliotekelezwa na maafisa wa polisi hususan katika vitongoji vinavyoshuhudia uhalifu mkubwa Nairobi.

Kumekuwa na hofu kuwa kifo hicho kimetokana na kazi zake ambazo jamii inaziona ni hatarishi kwa usalama na maisha.

Lakini taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai George Kinoti inasema kuwa makachero wanaamini mwanaharakati huyo alifariki wakati alipokuwa akitoa ujauzito Jumatano ya wiki iliyopita, (Februari, 6), siku ambayo alionekana kwa mara ya mwisho akiwa hai.

Caroline inaarifiwa ni mke na mama wa watoto wawili.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya wapelelezi, kuwa marehemu alikuwa kwenye mazungumzo ya simu ya mara kwa mara na mwanaume mwingine ambaye si mumewe kuhusu ujauzito huo. Polisi wanadai alikuwa ni mpenzi wake.

Mwanaume huyo, wapelelezi wanadai ndiye aliyefanya mazungumzo na kituo cha kutolea mimba kilichopo eneo la Dandora Phase I, Nairobi na kutoa kima cha Sh6,000 ili kazi hiyo ifanyike.

Baada ya kufikwa na umauti, polisi wanasema mwili wa Caroline ulipelekwa Nairobi City Mortuary saa 10 usiku ya Februari 7.

Watu sita, ikiwemo bwana huyo aliyekuwa akiwasiliana na marehemu, mmiliki wa kituo cha afya inachodaiwa alifariki ndani yake na dereva wa gari ya kukodi (Uber) wanashikiliwa na polisi mpaka sasa huku uchunguzi zaidi wa mkasa huo ukiendelea.
Hisia kali

Huu ni mkasa ambao umeacha hisia kali miongoni mwa Wakenya na makundi ya utetezi wa haki za binadamu.


Kampeni za kutaka kujua ukweli wa aliko bi Mwatha, ambaye kwa takriban wiki moja leo, alikuwa hajulikani aliko zilianzishwa katika mitandao ya kijamii.

Makundi ya kutetea haki za binaadamu likiwemo Amnesty International na hata mengine kama Missing Voices yalishinikiza kutafutwa kwa Bi Mwatha waliyemtaja kama "mtetezi wa dhati wa haki za binaadamu".

Kwa siku kadhaa kabla ya kupatikana kwa mwili wake familia na marafiki wa marehemu inaarifiwa walikuwa wakizunguka katika hospitali mbali mbali na hata vyumba vya kuhifadhia maiti wakimtafuta Carolina.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari Kenya, Caroline amekuwa akinakili visa vya mauaji yaliotekelezwa na maafisa wa polisi Kenya na visa vya watu kutoweka kiholela.

Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post