KILICHOENDELEA LEO MAHAKAMANI KESI YA MBOWE NA MATIKO

 Upande wa Mashtaka umewasilisha hoja mbili za rufaa katika Mahakama ya Rufani huku wakiomba rufaa namba 344 iliyopo Mahakama Kuu mbele ya Jaji Sam Rumanyika itupiliwe mbali kwa sababu haiendani na kifungu cha 362 (1) cha sheria ya Makosa ya Jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo rufaa ni lazima iambatanishwe na mwenendo wa kesi na uamuzi mdogo unaobishaniwa katika Mahakama Kuu lakini upande wa utetezi hawakufanya hivyo.

Rufaa hiyo ilikatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko.

DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kukubali kuendelea na usikilizwaji wa rufaa ya wabunge hao ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana.

Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi amedai leo Jumatatu Februari 18, 2019 mbele ya jopo la majaji watatu Stella Mgasha, Gerald Ndika, Mwanaisha Kwaliko wa Mahakama ya Rufani kuwa wanapinga uamuzi uliotolewa na Jaji Rumanyika katika rufaa namba 344 ya 2018 uliotolewa Novemba 30, 2018.

Akitoa hoja ya kwanza ya Rufani yao wakili Nchimbi amedai Jaji Rumanyika alipotoka kisheria kwa kuipanga na kuiita kwa ajili ya usikilizwaji huku akijua rufaa hiyo iliwasilishwa kinyume na kifungu cha 362 (1) cha sheria ya mwenendo wa Makosa ya jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo 2002.

Pia wanadai Jaji Rumanyika alijipotosha kwa kushindwa kuwapatia haki ya kutosha ya kusikilizwa.

Kwa upande wa Wakili Peter Kibatala alidai kuhusu lalamiko la kuwa hawakupewa muda wa kutosha wa kusikilizwa, rufaa iliyopo Mahakama Kuu haikusikilizwa na kwamba kilichosikilizwa ni mapingamizi pekee.

Hata hivyo, Jaji Mgasha kwa niaba ya jopo amesema watazingatia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili na kwamba watatoa uamuzi katika tarehe itakayopangwa.

Kibatala amedai sababu za rufaa hiyo hazina mashiko hivyo aliomba Mahakama ya Rufani kuitupilia mbali rufaa hiyo.

Mbowe na Matiko wamerejeshwa Segerea.

Na Tausi Ally, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527