WATUMISHI WA TFS WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA SHERIA

Mkurugenzi wa Huduma za Misitu Emanuel Wilfred (pichani) amewataka watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma na kujiepusha na kutenda kinyume kwenye utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza katika mkutano na wafanyakazi wa amakao makuu ya TFS jijini Dar es Salaam mapema hivi leo, Wilfred amesema TFS katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuhakikisha inasimamia rasilimali za misitu ili zisaidie katika uchumi wa taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho, imebaini kuwepo kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu miongoni mwa watumishi wake.

Amesema katika siku za hivi karibuni kumeibuka wimbi kubwa la watumishi wenye utendaji usioridhisha na wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma waliopo makao makuu na hata mikoani. 

“Sijawahi shuhudia watumishi wengi wakichukuliwa hatua za nidhamu kama mwaka huu. Watu wanafanya mambo yasiyovumilika yani utakuta mtumishi anatoweka tu kazini bila kutoa taarifa wala kuomba ruhusa! Mtumishi kutokuwepo kazini kwa siku tano bila ruhusa wala sababu za msingi adhabu yake ni kufukuzwa kazi. Sasa nawatangazia mtumishi yoyote atakayekosekana katika kituo chake cha kazi huku mwajiri wake hajui, atachukuliwa hatua” ,amesema.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo aliwataka watumishi ambao hawajaenda kwenye mafunzo ya Jeshi Usu kujiandaa kisaikologia kutokana na TFS kubadiri rasmi muundo wake na kuwa Jeshi Usu ambapo tayari watumiashi wa makao makuu wameanza utekelezaji wake.

Aidha, Mkurugenzi huyo aliwaeleza watumishi hao kuwa sambamba na mabadiriko hayo kuna marekebisho ya mishahara yanayoendelea ambapo tayari kuna baadhi wamepata mshahara mpya huku wengine wakiendelea kuhakikiwa ili wapate mshahara huo.

“Watu msiwe na wasiswasi najua wengine mshapata mishahara mipya huku wengine wakiwa hawajapata, waendelee kuwa wavumilivu taratibu za uhakiki zinaendelea na kwa miezi ambayo itakuwa hamjapata mtajaza fomu za madai ili kupata haki yenu,” alisema Mkurugenzi.
Mkurugenzi wa Huduma za Misitu Emanuel Wilfred (aliyesimama) akiwasisitizia watumishi wa TFS makao makuu (hawapo pichani) kufanya kazi kwa weredi kwenye utekelezaji wa majukumu yao leo 7 Februari 2019. Aliyekaa ni Mkurugenzi wa Rasilimali Misitu, Zawadi Mbwambo akifuatilia mkutano huo.
Wengine ni wafanyakazi wa TFS makao makuu wakifuatilia mkutano huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527