MASELE AJIGAMBA JINSI CCM ILIVYOSAMBARATISHA UPINZANI SHINYANGA

Mbunge wa Shinyanga (CCM), Steven Masele

Mbunge wa Shinyanga (CCM), Steven Masele amesema mkoa wa Shinyanga ulikuwa ngome ya wapinzani lakini wamefanikiwa kuisambaratisha.

Masele alisema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Alisema kwa kushirikiana na viongozi wa chama hicho wilaya na mkoa ndani ya kipindi cha miaka saba wamefanya kazi kubwa kuisambaratisha ngome hiyo na baadhi ya viongozi wa upinzani kuhamia CCM.

“Mheshimiwa makamu wa pili wa Rais waliokuwa miongoni mwa viongozi wa Chadema Shinyanga tuliokuwa tukipambana nao mwaka 2015 sasa hivi wamerudi nyumbani wamejiunga na CCM,” alisema.

 Masele alisema baadhi ya waliowahi kuwa viongozi wa Chadema ambao wamejiunga na CCM ni Hassan Baruti ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa baraza la vijana la chama hicho wilaya na Ngassa Donald aliyekuwa katibu wa mkoa wa Chadema.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Balozi Idd aliwataka wana CCM waachane na makundi ndani ya chama na badala yake washirikiane ili kuleta maendeleo wanayohitaji wananchi.

“Wana CCM lazima kuwa na nidhamu maana hatutasita kuwachukulia hatua wanaojifanya mchana wenzetu lakini usiku wanageuka.”

“Bora tuwe na wanachama wachache lakini wenye nidhamu na uchungu na chama, uchaguzi uliopita wapo wengi waliokwenda upande wa pili lakini walijirudi na baadhi yao waliomba radhi baada ya kubaini kosa,” alisema Balozi Idd ambaye ni mlezi wa CCM mkoa wa Shinyanga.

Naye katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Haula Kachwamba alisema jumla ya wanachama 40 wa vyama vyama vya upinzani wamejiunga na CCM, huku watu wengine zaidi ya 300 wakichukuwa kadi za kuwa wanachama wa chama hicho.

Na Stella Ibengwe, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527