WATOTO WAWILI MARAFIKI WANAOKAA DAWATI MOJA WAJIUA

 Kifo cha mtoto, Jasmine Ngole aliyejiua kwa kujipiga risasi hivi karibuni kinaendelea kusumbua akili za wazazi na walezi nchini.

Wakati kabla tukio hilo halijapoa, tukio jingine la watoto wawili kujiua kwa kujinyonga limetokea mkoani Manyara.

Katika tukio lisilo la kawaida, watoto wawili wa darasa la tano waliokuwa wakikaa dawati moja katika Shule ya Msingi Mikiroy wilayani Babati mkoani Manyara wamefariki dunia kwa kujinyonga katika matukio mawili tofauti.

Akizungumzia matukio hayo mjini Babati jana, kamanda wa polisi mkoa huo, Augostino Senga alisema la kwanza lilitokea juzi saa 11:00 jioni kwenye kata ya Magugu.

Alisema katika tukio hilo mtoto Mathayo Ezekiel (11) aliporudi nyumbani kwao jioni kutoka shule aliwakosa wazazi wake na kufuata funguo zilizokuwa zimehifadhiwa kwa jirani na baada ya kufungua mlango aliingia ndani na kujifungia chumbani ambapo alijinyonga kwa kutumia taulo hadi akapoteza maisha.

Alisema tukio la pili, mwanzoni mwanafunzi mwenzake alifariki dunia kwa kujinyonga kwa kanga.

Alisema mwanafunzi huyo Hamis Juma (11) ambaye alikuwa anasoma darasa la tano kwenye shule hiyo hiyo alifariki dunia kwa kujinyonga akiwa nyumbani kwao Magugu.

Ofisa mtendaji wa kata ya Magugu, Daniel Limbu alisema vifo hivyo vya watoto kujinyonga vimesababisha mshangao mkubwa kwa jamii katika eneo hilo.

Alisema Ezekiel alikuwa akiishi na mama yake na baba wa kambo baada ya mama yake kutengana na baba yake mzazi.

Na Joseph Lyimo, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527