WAVULANA WAINGILIWA KWA AHADI YA CHIPSI NA MIHOGO

Watoto wa kiume shule za msingi halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wapo hatarini kupata maambukizi ya Ukimwi na magonjwa ya zinaa kwa kurubuniwa na watu na kuwaingilia kimwili kwa ahadi ya kuwanunulia chipsi au mihogo.


Imetajwa kuwa hali ya kiafya kwa watoto wa kiume ni mbaya zaidi ikilinganishwa na wasichana, kutokana na ukweli kwamba nguvu kubwa imeelekezwa kwa wasichana ambao matokeo ya ushiriki wa ngono huonekana baadaye, baada ya kupata ujauzito.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Michael Mwandezi alikieleza kikao cha ushauri cha mkoa huo (RCC) kilichojadili masuala mbalimbali ikiwamo sekta ya elimu ambapo wanafunzi 214 wa shule za msingi na sekondari walipata ujauzito kwa kipindi cha Januari/ Septemba mwaka jana mkoani humo.

“Pamoja na kwamba lazima tuweke mipango madhubuti kuokoa watoto wa kike, lakini sasa hivi hali ni mbaya zaidi kwa watoto wa kiume hususani wale ambao hawali shuleni.... wanarubuniwa na kuingiliwa kimwili na watu waovu kwa malipo ya chipsi ama mihogo,” amesema.

Amesema katika kukabiliana na tabia hizo uchunguzi unaendelea kufanyika katika baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Moshi lakini katika hatua za awali, manispaa hiyo imelifanya suala la wanafunzi kula shuleni kuwa ni la lazima.

“Tumehimiza kamati za shule kuliweka suala la watoto kula shule liwe ni la lazima.... athari zake ni kubwa mno kwa watoto wetu, kwa sasa tunaweza tusilione kwa vile tunawatazama zaidi watoto wa kike, ila mkoa unahitaji kulitazama hili kwa jicho la tatu,”amesema.

Mkuu wa wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu alisema suala la mimba mashuleni linafuatiliwa kwa karibu ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa wapo baadhi ya watuhumiwa wamehukumiwa kwenda jela hadi miaka 30 kwa makosa ya kumpa mwanafunzi ujauzito.

Katika taarifa yake katika kikao hicho, Ofisa Elimu mkoani hapa, Yohana Ngowi, alisema suala la mimba mashule, linachukuliwa kwa uzito mkubwa na kwamba kwa kipindi cha mwaka 2017/2018 jumla ya watuhumiwa 97 wamefikishwa mahakamani kwa kuwapa wanafunzi ujauzito.

Hata hivyo, alisema tatizo hilo linachangiwa na kuporomoka kwa maadili ambapo baadhi ya wazazi na walezi kutotimiza wajibu wao na kutolea mfano kwa kipindi cha mwezi Septemba mwaka 2018 wanafunzi 60 wa shule ya sekondari ya kutwa Hai walibainika kujihusisha na ngono.
Na Nakajumo James - Moshi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post