WAHOFIA MAAMBUKIZI YA VVU KUPANDA BAADA YA KONDOMU KUADIMIKA


Kufuatia kushuka kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Mkoani Njombe kutoka asilimia 14 hadi asilimia 11.4 wananchi mkoani humo wamedai kuwa huenda kiwango hicho kikapanda tena kwa kile walichokidai kuwepo kwa upungufu wa upatikanaji wa Kondomu.

Hali hiyo inajiri siku chache baada ya Baraza la Madiwani katika halmashauri ya Mji Makambako kuwasilisha hoja ya upungufu wa kondom ambapo walimtaka Mkurugenzi kupitia Wizara ya Afya kuwasaidia wananchi kupata huduma hiyo.

Baadhi ya wananchi mkoani Njombe wamesema kutokana na jitihada za serikali juu ya kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kuna haja serikali kuangalia namna ya kuongeza kinga muhimu.

Nao baadhi ya wahudumu wa nyumba za kulala wageni na wafanyabiashara wa Kondomu wamesema ni miezi mitatu sasa tangu kuanza kuadimika kwa bidhaa hiyo jambo ambalo limepelekea wateja kuzifuata mbali na nyumba hizo za kulala wageni tena kwa bei kubwa.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Makambako Ernest Kyungu ametolea ufafanuzi juu ya changamoto hiyo na kubainisha kuwa serikali mkoani humo inaendelea kulifuatilia.

Chanzo- EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post