EWURA KUANZISHA VITUO VYA MAFUTA VYA KUHAMA HAMA


Na Amiri Kilagalila
Ili kurahisisha upatikanaji wa nishati ya mafuta mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji EWURA imesema kuwa inatarajia kuanzisha huduma ya sheli zinazotembea Mobile pump station kwa kutumia magari maalumu yalitengenezwa kwa kazi hiyo zikiwemo pikipiki za miguu mitatu zinazoendelea kuundwa kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM.

Mkurugenzi wa mawasiliano na mahusiano mamlaka ya udhibiti ya nishati na maji Taitas Kaguo ameyasema hayo wakati akijibu maswali ya baadhi ya wadau wa nishati na maji walioshiriki katika semina elekezi juu ya ufanyaji kazi wa mamlaka hiyo iliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Njombe mkoani hapo,pamoja na kutoa elimu ya misingi ya udhibiti wa nishati mafuta na maji huku akitambulisha ofisi mpya ya kanda iliyopo mkoani Mbeya.

Aidha amesisitiza kuwa nishati ya mafuta inatakiwa kuuzwa kwa utaratibu unaokubalika na kwa kujenga visima vikubwa ni gharama wanaona njia hiyo itakuwa ni rahisi kuwafikia wananchi wengi.

Amesema katika maeneo mengi hapa nchini wafanyabiashara wadogo wamekuwa wakisafirisha na kuuza mafuta kwa njia ambazo sio sahihi na zinazohatarisha usalama wa vyombo vya watumiaji pamoja na maisha yao wenyewe lakini hasa maeneo ya vijijini ambako hakuna vituo vya mafuta.

‘’Hata hivyo ewura tumejitahidi kukomesha tatizo la uchakachuaji wa mafuta ambalo lilikuwa limekithiri siku chache zilizopita lakini sasa limekwisha baada ya kutumia njia ya vina saba vya rangi pamoja na kupitia uagizaji wa mafuta kwa pamoja katika meli moja’’ aliongeza Kaguo.

Kaguo pia alishauri watumiaji vya vyombo vya moto kuacha kujaza mafuta katika vyombo vyao majira ya mchana kwa kuwa kuna kiasi cha mafuta hupotea kwa njia ya mvuke evaporation na kupelekea malalamiko ya kuwa wananyonywa na wahudumu au wamiliki wa vituo.

Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa kusafirisha au kuuza mafuta kwa njia zisizo rasmi kwa kutumia madumu ni kosa kisheria na pia hatari kubwa inayoweza kusababisha majanga kama milipiko ya moto.

‘’Kutokana na ongezeko la vyombo vya usafiri kama pikipiki tumeamua kupunguza gharama za kuanzisha vituo vya uuzaji mafuta ili viweze kujengwa katika maeneo mbalimbali hasa vijijini ili kuepuka uuzaji mafuta katika vidumu",amesema Kaguo.

Baadhi ya wadau wengine walioshiriki semina hiyo wameitaka mamlaka kuhakikisha inatatua changamoto za mafuta na maji hasa kupanda holela kwa bei katika maeneo ya vijijini kwa kisingizio cha umbali.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Chiristopher Ole Sendeka ndiye aliyefungua na kufunga mkutano huo aliwapongeza ewura kwa kuanzisha ofisi za kanda ambazo zitahudumu mikoa ya njombe ,Ruvuma, Mbeya, na Katavi kwa kuwa wamesogeza huduma karibu na wakazi wa mikoa hiyo na kurahisisha uwasilishaji wa matatizo yao.

‘’ Nawapongeza EWURA makao makuu kwa kuona umuhimu wa kuanzisha ofisi ya kanda nyanda za juu kusini na nimeona mmekuwa mkija ofisi kwangu mara nyingi hii itasaidia kuwafundisha watu wetu kuzingatia kanuni na taratibu zinazohusu nishati na maji’’, amesema Ole Sendeka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527