Raia mmoja wa Niger ambaye amefukuzwa nchini Israeli amenasa uwanja wa ndege nchini Ethiopia toka mwezi Novemba mwaka jana.
Eissa Muhammad (24), amenasa kwenye kiwanja hicho jijini Addis Ababa baada ya nchi yake kugoma kumpokea.
"Nimekuwa nikikaa hapa (uwanja wa ndege) katika mazingira magumu, hakuna kitu, hakuna kitu kabisa..." Muhamad ameiambia BBC.
Mikasa ilianza kumuandama Muhamad Aprili mwaka jana baada ya kunaswa akiishi nchini Israeli bila ya kibali, imeelezwa kwamba kijana huyo alihamia Israeli kutoka Niger mwaka 2011, akiwa na miaka 16 ili kutafuta maisha bora.
Amesimulia kwamba aliwalipa wasafirishaji wa binaadamu ili kumpitisha nchini Libya na Misri kabla ya kuingia Israeli kwa miguu, na alipofika jijini Tel Aviv, Muhamad aliishi kwa kutegemea kazi duni kwenye majumba ya kuishi wanafunzi na kiwanda cha kuzalisha pipi.
Baada ya kushikiliwa kizuizini kwa zaidi ya miezi sita, Israeli ilimpatia hati ya dharura ya kusafiri na kumpakia kwenye ndege ya Shirika la Ethiopia kuelekea Niger kupitia Addis Ababa mwezi Novemba.