MASHAHIDI 15 KUTOA USHAHIDI KESI YA UCHOCHEZI INAYOMKABILI ZITTO KABWE

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam inatarajia kuanza kusikiliza ushahidi wa mashahidi 15 katika kesi ya uchochezi na kusababisha chuki ndani ya jamii inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

Hatua hiyo ilifikiwa na mahakama hiyo Dar es Salaam jana kesi hiyo ilipopelekwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa Serikali Adofu Kisima, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kuiomba kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa.

Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 29, mwaka huu na mshtakiwa yuko nje kwa dhamana.

Zitto ambaye ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, anadaiwa kuwa Oktoba 28, mwaka jana, maeneo ya Kijitonyama wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, aliitisha mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho kwa lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwamba kinyume na sheria alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Anadaiwa kutamka kuwa; “watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post