NAIBU WAZIRI WA MADINI AAGIZA WAMILIKI WA MGODI KUKAMATWA

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameamuru kukamatwa kwa Wamiliki wa mgodi wa Nyakavangala unaomilikiwa na Thomas Masuka and Partners kufuatia wamiliki hao kutofautiana juu ya taarifa waliyoiwasilisha kwa Naibu Waziri kuhusu namna mgodi huo unavyoendeshwa ikiwemo ulipaji wa kodi na mrabaha wa serikali.


Naibu waziri amewataka wamiliki hao kutoa maelezo ya kina kuhusu ni lini watalipa kodi zote wanazodaiwa na serikali baada ya kuonekana kuwa mgodi huo unadaiwa zaidi ya shilingi milioni 128 za mrabaha ambazo imedaiwa kuwa, wapo baadhi ya wamiliki ambao wamekuwa wakikusanya fedha hizo lakini zimekuwa hazilipwi.

Katika ziara yake mkoani humo, Naibu Waziri alisema kuwa pamoja na kujionea shughuli za uchimbaji katika migodi ya dhahabu ya Ulata na Nyakavangala, amebaini ukwepaji mkubwa wa kodi pamoja na mrabaha wa serikali.

Amemtaka Afisa madini kutoa maelekezo ya kina kuhusu suala zima la ulipwaji wa kodi na mrabaha wa serikali, huku akiagiza zoezi hilo pia limuhusishe Afisa Msimamizi wa madini aliyekuwepo katika kipindi ambacho fedha hizo hazikulipwa.

Hatutaki ugomvi hapa kwenye migodi. Tunataka mgodi ufanye kazi. Dhahabu ziuzwe mahali panapoonekana. Hapa naona hesabu za viroba tu. Mnunuzi wa dhahabu hapa ni nani”, alihoji Naibu Waziri Nyongo.

Wakati akizungumza na wachimbaji katika mkutano wa hadhara, amewataka wachimbaji hao kuchimba kwa kuzingatia usalama huku akisisitiza suala la kufuata sheria na taratibu huku akiwataka kutoa taarifa za uhakika kwa wale wote wanaokikuka sheria ikiwemo watoroshaji wa madini huku akisisitiza utoaji taarifa hizo usiwe wa majungu.

 Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliwataka wamiliki hao kukaa chini na kukubaliana namna ya kulipa kiasi cha fedha ambacho wanadaiwa na serikali huku akimtaka afisa kutoka halmashauri anayehusika na masuala ya usimamizi wa fedha kuhakikisha kwamba fedha ambazo mgodi huo ulipaswa kuzilipa kama mrabaha zinapatikana.

Mgodi huo wa Nyakavangala unamilikiwa na Thomas Masuka kwa ushirikiano na wawekezaji wengine wazawa wapatao 20. Wakati akiagiza kukamatwa kwao, wamiliki 8 kati ya 20 ndiyo walikuwa wamehudhuria kikao kati yake na wamiliki hao.

Naibu Waziri Nyongo alitoa agizo hilo Januari 15 wakati akihitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani humo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527