WADAU WA SOKA SHINYANGA WALIA NA TFF UKATA VILABUNI


Wadau wa soka Mkoani Shinyanga wameliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini(TFF) kuvinusuru vilabu vinavyoshiriki ligi kuu soka Tanzania bara,kwa kutafuta mdhamini mkuu atakayeondoa hali ya ukata kwa vilabu shiriki katika mzunguko wa pili msimu huu wa 2018/19. 


Wakati baadhi ya timu zinazoshiriki ligi kuu soka Tanzania bara zikiwa zimemaliza mzunguko wa kwanza wadau wa michezo hasa soka mkoa wa Shinyanga wamezungumza na Malunde 1 blog katika maeneo tofauti mkoani hapa na kutoa tathmini ya mwenendo wa ligi hiyo hasa hali ya kiuchumi kutokana na timu nyingi kumaliza mzunguko huo zikiwa hohe hahe. 

Alfred Peter ni miongoni mwa wadau wa soka mkoani hapa ambaye pia ni mwanachama wa timu ya Stand United amesema pamoja na ligi kwenda vizuri kutokana na mpangilio wa shirikisho la soka nchini kuongeza timu nne,lakini ukosefu wa mdhamini mkuu wa ligi kumesababisha vilabu vingi kusindwa kujiendesha ikiwa ni pamoja na kukimbiwa na wachezaji. 

“Wachezaji wengi wamekimbilia timu zenye ahueni kiuchumi kutokana na ukata unaozikabili timu nyingi shiriki za ligi kuu nahii imesababishwa na ukosefu wa mdhamini mkuu kwenye ligi hii” Alisema Peter. 

Wadau hao wamesema endapo hali ya kukosa mdhamini mkuu wa ligi kuu soka tanzania bara msimu huu ikiendelea katika mzunguko wa pili wanahofia kuibuka kwa upatikanaji wa matokeo ya mezani kutokana na ukosefu wa fedha na kuliomba shirikisho la mpira wa miguu nchini tff kufanya jambo kuzinusuru timu hizo na kadhia hiyo. 

Ligi kuu soka Tanania bara msimu huu wa 2018/19 imeendeshwa bila mdhamini mkuu huku vilabu shiriki vikiwa na hali mbaya kiuchumi ambapo ligi hiyo awali ilikuwa ikidhaminiwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom ambayo ilikuwa ikitoa fedha taslimu zaidi ya shilingi za kitanzania milioni 100 kwa timu shiriki jambo ambalo limekosekana msimu huu.

Na Malaki Philipo,  Malunde 1 blog.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527