WAFANYAKAZI WAANDAMANA KISA MAGUFULI



Wafanyakazi wakiwa wameshika mabango yenye maneno ya kumpongeza Rais, Magufuli.

Wafanyakazi jijini Dar es salaam wameandamana kwa lengo la kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kufuta kikokotoo kipya cha mifuko ya hifadhi za jamii na kurejesha cha zamani.

Maandamano hayo yamefanyika leo, Januari 3,2019 ambapo yameanzia ofisi za Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Mnazi Mmoja jijini humo hadi viwanja vya Mnazi Mmoja wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kumpongeza Rais Magufuli, yamepokewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva.

Akizungumza na waandamanaji hao, Lyaviva ametoa rai kwa wafanyakazi wa umma nchini kufanya kazi kwa uadilifu na kuwahudumia wananchi bila upendeleo. Amesema wapo baadhi ya watumishi wa serikali wanaochelewesha huduma kwa wananchi kwa makusudi hali inayosababisha malalamiko.

“Zingatieni nidhamu ya utumishi na utendaji, bahati nzuri kila taasisi ina mfumo wake wa utendaji kazi zingatieni hiyo mifumo, furaha hii ya kikokotoo haimanishi mjisahau katika kuwahudumia wananchi,” amesema.

Akizungumzia kuhusu tamko la Rais Magufuli la kusitisha kikokotoo walichokiita kandamizi amesema uamuzi huo uwe chachu ndani ya mioyo ya wafanyakazi hao kwa kufanya kazi kwa bidii na kujituma zaidi.

Akisoma risala iliyoandaliwa na wafanyakazi hao, Katibu wa kamati za wanawake wa TUCTA, Jenijely James amesema kikokotoo hicho kilichorejeshwa kina mafao bora katika sekta ya umma.

Desema 28, 2018, Rais Magufuli alikutana na TUCTA, viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na wadau wengine Ikulu jijini Dar es salaam na kusitisha kikokotoo kipya na kurudisha cha zamani ambacho kitatumika hadi 2023.
Chanzo - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527