TADB, NFRA WAWAHAKIKISHIA WAKULIMA SOKO LA MAHINDI


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kushirikiana na Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA), wameingia makubaliano kuongeza thamani ya mnyororo wa thamani wa zao la mahindi kwa kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanapata soko la uhakika ili waweze kunufaika na kilimo.

Akizungumza baada ya kumaliza kikao cha pamoja, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, alisema wamekubaliana na NFRA kuhakikisha zao la mahindi linapata soko, jambo litakalompa uhakika mkulima kuendelea na kilimo cha zao hilo.

“TADB ilishatoa zaidi ya Sh. bilioni 3.4 kwa vikundi 22 vya wakulima katika kufanya kilimo cha kisasa cha zao la mahindi, hivyo kupitia kikao hiki tunawahakikishia wakulima wa mahindi soko la uhakika,” alisema Justine.

Alisema kwa msimu wa kilimo uliopita soko la zao la mahindi liliyumba, hivyo kupitia mazungumzo kati ya TADB na NFRA yataibua matumaini kwa wakulima wengi wa mahindi kwa kupata soko la bidhaa hiyo ambayo bei yake ilishuka kutokana na uzalishaji kuongezeka tofauti na mahitaji ya nchi.

“Pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kununua zaidi ya tani 36,000 za mahindi bado shehena nyingi za mahindi zipo kwa wakulima, hivyo kama wadau wa sekta ya kilimo ni wajibu wetu kuhakikisha shehena hizo zinapata soko,” alisema.

Justine alisisitiza kuwa ili kumfanya mkulima kuendelea na kilimo cha zao hilo ni lazima ahakikishiwe soko la bidhaa yake itakayompa hamasa ya kulima kwa tija ili aweze kupata mavuno kwa wingi na tija inayotakiwa sokoni.

“TADB itaanda mkakati wa pamoja na NFRA utakaoleta mabadiliko makubwa katika mnyororo wa thamani wa zao la mahindi nchini, hii ni kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika msimu wa kilimo uliopita ulifanya zao la mahindi kushuka thamani,” alisema Justine.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia Zikankuba, alisema wamefanya mazungumzo mazuri na TADB ambayo yatawasaidia kama wakala katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha zao la mahindi linapata soko.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527