SERIKALI YAPIGA 'STOP' BOMOA BOMOA KWENYE MAKAZI YASIYO RASMI

Rais, John Pombe Magufuli.

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametoa fursa kwa wananchi waliojenga bila ya kufuata mipango miji na hawana hatimiliki za ardhi kufanyiwa urasimishaji wa makazi na kuelekeza kuwa wasibomolewe nyumba zao tena kwakuwa hayakuwa makosa yao kujenga maeneo hayo.

Hayo yamesema na Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, William Lukuvi, wilayani Simanjiro mkoani Manyara alipofanya ziara ya kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi kwa wakazi wa mji huo, ambapo amewataka wananchi wote wachangamkie fursa hiyo iliyotolewa na Rais.

Amesema kwamba Serikali ya awamu ya tano kuanzia sasa haitabomoa tena nyumba za wananchi waliojenga maeneo ya makazi yasiyo rasmi badala yake itarasimisha makazi holela.

“Serikali ya awamu ya tano inajali sana wananchi wake kwakuwa zamani wananchi ambao hawakujenga kwa kufuata mipango miji wangebomolewa nyumba zao, lakini kwa sasa imeanzisha mpango kurasimisha makazi holela na kuwapatia hati wananchi wote waishio mijini ili waishi katika makazi rasmi”, amesema Lukuvi.

Pamoja na hayo Lukuvi amewataka wananchi wote waishio mijini kuwa wazalendo kwa kurasimisha maeneo yao waweze kujipatia hati na ili walipe kodi ya pango la ardhi jambo ambalo litaiongezea Serikali mapato.

Chanzo:Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527