PICHA ZA ALIYEPOTEA ZASAMBAA MTANDAONI AKIWA UCHI KAVAA SHANGA



Matukio ya kutoweka kwa wananchi sasa yanazidi kuibuka baada ya kijana mmoja mkazi wa kijiji cha Michungwani wilayani Handeni kupotea na siku chache baadaye picha zinazomuonyesha akiwa hana nguo na amevaa shanga, zinasambaa katika mitandao ya kijamii.

Kijana huyo Omari Athumani, ambaye ni dereva wa gari la mfanyabiashara aitwaye Ally Matahika, maarufu zaidi kwa jina la Kanto, alitoweka Novemba 14 mwaka jana baada ya kumuaga mama yake kuwa anakwenda kupakia mzigo wa machungwa, na hadi sasa hajaonekana.

Bado sababu za kutoweka kwake hazijajulikana, lakini mkuu wa kituo cha polisi Michungwani, Mgaza Mnkangara amesema kijana huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa tajiri yake anayeitwa Kanto na kusisitiza kwamba “mwanamke anauma”.

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tuhuma hizo, Kanto alisema anafahamu kuhusu kutoweka kwa Omary lakini amekataa kuzungumzia suala hilo kwa undani.

“Ni kweli,” alijibu Kanto alipoulizwa kama ana taarifa za kupotea kwa kijana huyo, lakini alipoulizwa kuhusu kudhalilishwa kwa kijana huyo na picha zake kusambaa mitandaoni, alikataa kuzungumzia suala hilo.

“Mimi kwa sasa sitaki kuzungumzia suala hilo,” alisema.

Mkuu wa wilaya, kamanda wa polisi wa wilaya na mwenyekiti wa kijiji, wote wana taarifa za kutoweka kwa Omary, lakini wameshindwa kumuhusisha tajiri wake na kitendo cha kutoweka na kudhalilishwa kwa kijana huyo na kwamba uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post