AUAWA KWA KUKATWA PANGA NA RAFIKI YAKE KISA KAMTANIA KWA KUMUITA 'ALBINO'

Mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya sekondari Naisinyai wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara Godfrey Otieno (16) amefariki dunia kwa kukatwa panga kichwani na rafiki yake baada ya kumtania kwa kumuita albino.

Watoto hao ambao ni marafiki na majirani walikuwa pamoja wakisubiria kushangilia mwaka mpya wa 2019 ambao uligeuka kuwa kilio.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, Agostino Senga akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Januari 2, 2019 amesema tukio hilo limetokea Desemba 31, 2018 saa tatu usiku katika kitongoji cha Songambele kata ya Mirerani wilayani Simanjiro.

Amemtaja anayedaiwa kufanya mauaji hayo ni George Damas (15) mwanafunzi aliyemaliza shule ya msingi hivi karibuni na kufaulu, alikuwa akisubiri kupangiwa shule ya sekondari.

Ametaja chanzo cha kifo hicho ni utani kwani Otieno alimtania mwenzake kwa kumwita albino ndipo akakasirika na kuchukua panga na kumkata kichwani.

"Baada ya Otieno kukatwa na panga alikimbizwa kwenye kituo cha afya Mirerani lakini alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu," amesema kamanda Senga.

Amesema wanamshikilia Damas huku wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kumfikisha mahakamani.

Na Joseph Lyimo, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post