RAIS MAGUFULI AWAUMBUA VIONGOZI WANAOSINGIZIA 'NI MAAGIZO KUTOKA JUU'

Rais John Magufuli juzi usiku alitoa salamu za mwaka mpya wa 2019 kwa kuhoji tabia ya watumishi wa umma kutojiamini katika utendaji wao wa kazi kiasi cha kila jambo wanalolifanya kudai kuwa “ni maagizo kutoka juu”, akisema neno hilo sasa limekuwa kama ugonjwa.

Kauli hiyo ya Rais imekuja kipindi ambacho watendaji mbalimbali serikalini wamekuwa wakitumia neno hilo katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa masuala yanayowahusu wananchi.

Akizungumza dakika chache kabla ya kufika saa 6:00 usiku juzi, Rais Magufuli alisema, “Na mara nyingi maagizo yanakuwa hayapo, bali ni utekelezaji wa wajibu wa sheria, wajiamini na wasiwaonee watu lakini watimize wajibu wao.”

Mbali na kuwataka watendaji serikalini kujiamini, Rais Magufuli alisema mwaka huu utakuwa wa mafanikio zaidi kiuchumi na kuwataka Watanzania kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano.

“Ujumbe wangu kwa watumishi wa umma, ni kama nilivyotoa ujumbe kwa Watanzania wengine, wachape kazi, wajiamini,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:


“Waachane na utamaduni wa kila kitu wanachokifanya kudai ni maagizo kutoka juu, huo ni ugonjwa ambao umeanza kuwapata watumishi wa umma ambapo kila wanalolifanya hata kama ni kwa mujibu wa sheria hawataki kujiamini, na wanasema hili ni maagizo kutoka juu.”Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post