OJADACT YAJITOSA SAKATA LA MUSWADA WA VYAMA VYA SIASA TANZANIA

Chama cha Waandishi wa Habari wa Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT), tunachukua nafasi hii kuwakaribisha kwenye mkutano huu wenye nia ya kutoa uelewa wa muswada wa vyama vya siasa Nchini pamoja na maoni ya wadau mbalimbali waliokwishatoa maoni yao sanjali na kupokea maoni yenu kama wana taaluma na wadau wa habari.

  

Ndugu Waandishi wa habari kama mjuavyo kwa sasa kumekuwa na mikutano mbalimbali kwa kada mbalimbali juu ya kutoa maoni yao kuhusu muswada wa vyama vya siasa Nchini, tumeshuhudia makundi ya kitaaluma na makundi mengine katika jamii, kama wanasheria, wafuasi wa vyama vya siasa, wanafunzi na wanazuoni, wote wakitoa maoni juu ya muswada huu.

Licha ya maoni hayo yote kutolewa, bado vyombo vya habari ndivyo vinavyotegemewa sana kwenye kuelimisha umma juu ya muswada huo, lakini swali kubwa limebaki ni kwa namna gani waandishi wa habari wamejengewa uwezo wa kuujua na kuutafsiri vyema a muswada huo ili waweze kuyapima na kuyatafakari maoni yaliyotolewa na kada mbalimbali Nchini?.

Jambo hili linatupa wasiwasi na tunaamini waandishi wa habari walipaswa kufafanuliwa vyema muswada huu kabla ya maoni ili waweze kuandika vyema maoni ya kitaifa baada ya wao kuujua muswada kwanza. 

Hivyo basi OJADACT, inasukumwa na sababu kuu mbili za kuwa na mkutano wa januari 21 mwak huu, kwanza ni kuwawezesha waandishi wa habari kuuelewa muswada huu ili waweze kuandika habari zenye maudhui ya muswada wa vyama vya siasa kwa weledi Zaidi na kujibu kiu ya walaji wa habari bila kuacha maswali. 

Lakini sababu ya pili ni kuwapa nafasi waandishi wa habari na wadau wa habari kupata fursa ya kutoa maoni yao na kuwasilishwa katika kamati maalumu Bungeni ili maoni hayo yazingatiwe kwenye maboresho ya muswada huo, kama walivyofanya wanataaluma pamoja na makundi mengine, kama tujuavyo suala la siasa ni suala mtambuka na linagusa maisha ya kila siku ya binadamu. Hivyo ni fursa sasa kwetu kutoa maoni yetu. 

Hivyo OJADACT imeandaa siku maalumu ambayo ni Januari 21, 2019 ambapo kutakuwa na mkutano wa kuueleza kwa ufasafa maudhui ya muswada huo na pia kupata maoni toka kwenu na wadau wa habari, sehemu ambayo mkutano huo utafanyika ni katika hotel ya Gold Crest iliyopo hapa Jijini Mwanza, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 4:30 ambapo tutahitimisha zoezi hilo. 

Baada ya hapo tutaandika vizuri maoni ya waandishi wa habari na kuyapeleka Bungeni Jijini Dodoma. Hivyo basi tunawakaribisha wanahari wote, wadau wa habari pamoja na wananchi wengine kuhudhuri mkutano huo. Watoa mada mahiri wenye weledi wa kisheria na habari toka vyuo vya kihabari watakuwepo ili kuwapitisha kwenye maeneo muhimu ya muswada huo. 
Ahsanteni
Edwin Soko
Mwenyekiti-OJADACT

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527