MAKOSA 12 WALIYOSOMEWA POLISI NA WATUHUMIWA WALIOKUWA WAKITOROSHA DHAHABU MWANZA

Askari polisi wanane wanaotuhumiwa kushiriki mpango wa kutorosha dhahabu kilo 319.59 zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 27 pamoja na wamiliki wa madini hayo, wamefikishwa mahakamani.


Washtakiwa hao waliokamatwa Januari 4, mwaka huu, walifikishwa mahakamani kwa makosa 12 likiwemo la uhujumu uchumi.


Walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Gwae Sumaye, na mawakili wa serikali Castuse Ndamgoba, Robert Kidando na Jackline Nyantori.


Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Januari 4, watuhumiwa wanne ambao ni Sajid Abdallah, Kisabo Nkinda, Emmanuel Kija na Hassan Sadick walitenda kosa la kuwapatia rushwa ya Sh. milioni 700 watuhumiwa wanne ambao ni askari polisi ili kuwasaidia kutorosha madini hayo.


Askari ambao majina yao yalitajwa na mawakili wa serikali ni Koplo Dani Kasara, Koplo Matete Misana na makonstebo Japhet Kuliko, Maingu Sorry, Alex Mkali, Timoth Paul na David Ngelela na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Moris Okinda ambaye alikuwa kiongozi wa askari hao.


Miongoni mwa mashtaka 12 yanayowakabili askari hao ni pamoja na uhujumu uchumi, kuomba na kupokea rushwa ya Sh. milioni 700, kuisababishia hasara serikali na kutakatisha fedha kinyume cha sheria za nchi.


Hakimu Gwae alisema watuhumiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 28, mwaka huu, itakapotajwa.


Askari hao wanane, kabla ya kufikishwa mahakamani, Jeshi la Polisi Tanzania liliwasimamisha kazi Januari jana kutokana na tuhuma za kutenda kosa kinyume cha mwenendo mwema wa jeshi hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527