HAWA NDIYO MAKOCHA 7 WENYE NAFASI YA KUTUA MAN UNITED


OLE Gunnar Solskjaer amepewa nafasi kama kocha wa muda wa Manchester United baada ya kufukuzwa kwa Jose Mourinho hapo kwenye dimba la Old Trafford.

Pamoja na kwamba Solskjaer ameanza vizuri kwenye kikosi hicho kwa kushinda mechi zake zote tano za mwanzo, lakini bado kuna majina yanayotajwa kuwa yanafaa kupewa nafasi ya ukocha hapo United.

Hapa tunawachambua makocha saba wanaopewa nafasi ya kuchukua mikoba ya kuiongoza klabu hiyo.

7. Antonio Conte

Ni mmoja wa majina yanayotajwa zaidi, hasa baada ya kuwa tayari ameshawahi kushinda taji la Ligi Kuu England. Tangu alipochukua nafasi ya kuinoa Juventus mwaka 2011, Conte ameshinda mataji sita katika miaka saba. Kama United wakitaka mtu ambaye atawarudisha kwenye utamaduni wao wa kushinda, basi Conte ana nafasi.

6. Eddie Howe

Howe amekuwa mmoja wa makocha wenye sifa nzuri zaidi katika historia ya soka la Uingereza kwa miaka ya hivi karibuni, kwa kuwa ameweza kuiongoza Bournemouth kutoka ligi daraja la chini na kuipandisha hadi Ligi Kuu, huku pia amewahi kuitumikia kwa muda mfupi.

Anaweza asiwe na gharama kubwa kumpata, kwa sababu anaijua vizuri ligi hiyo na haiba yake ni nzuri zaidi kwa wachezaji. Kikubwa zaidi ni kwamba bado kijana, katika umri wake wa miaka 41, anaweza kuwa chaguo sahihi zaidi kwa United kwa sasa.

5. Laurent Blanc

Blanc ana uzoefu wa kutosha kwenye kufundisha soka katika ngazi ya juu zaidi, na inasemwa kwamba yeye ndio sababu ya PSG kutawala soka la Ufaransa na Ligi Kuu ya nchi hiyo. Kwa kuwa alifanya makubwa kuijenga timu hiyo baada ya kurithi mikoba kutoka kwa Carlo Ancelotti. Kwa sasa yupo huru na anaweza kurudi kwenye nafasi ya ukocha kwa kuifikisha mbali United. 

4. Massimilliano Allegri

Ameshinda kila kitu kwenye ardhi ya nyumbani kwake Italia akiwa na Juventus, hivyo kama United wanataka kuendeleza utamaduni wao wa kushinda kila kitu, Massimilliano ndio anafaa kubebeshwa mikoba ya hapo Old Trafford. Taji pekee ambalo hajashinda na Juventus ni la Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo iwapo atatua hapo Man United anaweza kupata changamoto nzuri na pengine hata kulibeba taji hilo. 

3. Zinedine Zidane

Zidane amechukua likizo kwenye kazi ya ukocha baada ya kuondoka pale Real Madrid wakati wa kipindi cha majira ya joto na alitarajiwa kwamba angerudi haraka. Man United anaweza kuwafaa, kwa kuwa Zidane nae ana molari ya kushinda na kama atatua hapo anaweza kuwa msaada mkubwa kwao.

Tayari mafanikio yake ya muda mfupi pale Real Madrid yanaweza kuwa chachu nzuri zaidi ya kuisaidia Man United. 

2. Ole Gunnar Solskjaer

Tayari anapendwa na mashabiki wa Man United na hasa kutoka na historia yake wakati akiichezea klabu hiyo kwa miaka 11. Tangu amechukua mikoba ya kuinoa timu hiyo kwa muda hadi mwishoni mwa msimu, tayari ameshinda mechi zote tano (kabla ya mechi ya jana wikendi). Anaonekana kama kocha anayeelewana zaidi na wachezaji na kwa uhakika anaweza kuifikisha United mahali panapotakiwa.

1. Mauricio Pochettino

Mashabiki wa Tottenham Hotspurs wana kila sababu ya kuchukizwa na habari kwamba kocha wao anawaniwa na klabu kadhaa kubwa Ulaya na hii ni kutokana na mafanikio aliyonayo kwenye klabu yao. Tangu ametua hapo Spurs kocha huyu raia wa Argentina ameiongoza timu hiyo kutokuwa nje ya tano bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu na hayo ni mafanikio makubwa zaidi kwa kikosi hicho.

Kwa vyovyote vile, Pochettino ana nafasi nzuri zaidi ya kusaidia Man United kuweza kurudi kwenye enzi zake za gwiji Sir Alex Ferguson katika kutawala soka la Uingereza na hata Ulaya. 

Pochettino ana nafasi ya kuifanya tena United kuwa fahari ya soka la Uingereza, ambapo kwa miaka ya hivi karibuni imeonekana kama kiwango chake kimeporomoka.

Hivyo kama kocha huyo atapewa nafasi hapo Old Trafford kuna uwezekano mkubwa kuifanya timu hiyo kurudi kwenye kiwango chake kilichozoeleka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527