Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameanza ziara barani Ulaya na leo atakuwa London, Uingereza ambako amesema ataeleza kwa kina kile alichoandika katika waraka aliotoa kwa ajili ya mwaka huu.
Ziara ya Lissu inaanza baada ya Desemba 31, mwaka jana kuhitimisha safari ya matibabu aliyoanza Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa zaidi ya risasi 30 mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha mchana cha Bunge.
Akizungumza na Mwananchi jana, Lissu ambaye hivi karibuni ameeleza nia yake ya kugombea urais kupitia Chadema, alisema leo ataitikia mwaliko wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Lissu alikwenda Ubelgiji Januari 6 mwaka jana kuendelea na matibabu akitokea Hospitali ya Nairobi, Kenya na katika kipindi chote cha matibabu, amefanyiwa upasuaji mara 22.
Alisema baada ya kutoka Uingereza, amepata mwaliko mwingine wa kwenda katika ofisi za Umoja wa Ulaya (EU) zilizopo Brussels, Ubelgiji na baadaye ataelekea Marekani na katika ziara hizo amesema ataelezea kile kilichomtokea Septemba 7, 2017, hali ya kisiasa nchini na mambo mengine.
Katika waraka wake huo alioutoa Januari 5, Lissu alitaja matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu huku pia akihoji sababu ya Bunge kutogharamia matibabu yake, mambo ambayo pia amesema kwamba atayaeleza katika ziara yake hiyo.
Waraka huo wenye kichwa cha habari ‘Mwaka mpya 2019, Mwaka wa kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu wetu Tanzania’ umegusia pia masuala ya haki za binadamu yakiwamo matukio ya utekaji, mauaji na mashambulio ya kudhuru mwili.
Mbali na kudai gharama za matibabu, Lissu amelalamika kutotembelewa na Spika Job Ndugai wala watumishi wa Bunge tangu alipolazwa hospitali licha ya kuwapo kwa ahadi hiyo.
“Kabla sijahamishiwa nchini Ubelgiji kutoka Kenya, Spika Ndugai aliahidi hadharani, kwenye mahojiano na Azam TV, kwamba atafika kunitembelea, mahali popote nitakapokuwa nimelazwa hospitalini.
“Hadi ninapoandika maneno haya, bado Spika Ndugai hajatimiza ahadi yake hiyo. Na hadi sasa, hakuna mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, au afisa yeyote wa Bunge, aliyefika hospitalini kuniona na kunijulia hali,” ameandika Lissu katika waraka wake.
Hata hivyo, Spika Ndugai alijibu madai hayo ya Lissu akimtaka arejee nchini waweke mambo mezani kisha Watanzania wapime nani asiye na shukrani.
Alisema alipanga kwenda kumtembelea Nairobi lakini, “tarehe zangu nilizokuwa nimezipanga, akawa amehamishiwa kwenda Ubeligiji, kwa hiyo safari yote ikawa imevurugika.”
Kuhusu Bunge kugharamia matibabu yake, alisema ni kwa sababu hakufuata utaratibu unaotakiwa kwa mbunge kutibiwa nje.
“Mbunge hatibiwi katika nchi anayotaka mwenyewe kama yeye anavyofanya, unatibiwa nje pale inapobidi, pale unapokuwa na recommendations (ushauri) ya madaktari bingwa watatu wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.
Chanzo - Mwananchi