MAHAKAMA KUU YATUPILIA MBALI KESI YA ZITTO KABWE NA WENZAKE

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeifuta kesi iliyofunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo na wenzake wa vyama vya upinzani waliyokuwa wakiitaka mahakama hiyo kuzuia kusomwa kwa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wakidai kuwa uko kinyume na katiba ya nchi.

Mahakama imetoa uamuzi huo leo Jumatatu, Januari 14, 2018 ambapo walalamikaji, Zitto na wenzake wamekubali maamuzi hayo na kusema sasa nguvu yao ni kwenda kuupinga muswada huo kwenye kamati za bunge.

Jaji Benhajo Masoud amesema Mahakama imeliondoa shauri hilo baada ya waombaji kuchanganya mashataka mawili kwa pamoja.

“Mahakama imeondoa shauri letu dhidi ya serikali kupinga muswada wa sheria ya vyama vya siasa na kifungu cha 8(3) cha sheria ya Haki na Wajibu ( BRADEA ) kwa sababu ya maombi hayo mawili kuunganishwa. Kufuatia uamuzi huo wa mahakama tumeagiza mawakili leo wafungue kesi mpya ya BRADEA.

“Tunaheshimu maamuzi ya mahakama na tunaamini mahakama imetenda haki. Hivyo tumeamua kurudi mahakamani kwa ombi moja la kupinga kifungu cha 8(3) cha sheria ya Haki na Wajibu. Kifungu hiki kinakiuka katiba kwa kuzuia mashauri ya kupinga miswada ya sheria. Mahakama ni chombo cha haki.

“Tutaendelea kuupinga muswada wa sheria ya kurekebisha sheria ya vyama vya siasa mbele ya kamati za bunge na ndani ya bunge. Muswada ukipita kuwa sheria kama ulivyo au kuwa mbaya zaidi, tutaupinga mahakamani tena. Hatutakata tamaa katika kudai haki,” amesema Zitto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post