BINTI AJINYONGA KISA KAZUIWA KWENDA KWENYE MKESHA WA MWAKA MPYA


Mwaka Mpya wa 2019 umeanza na visa vya watu wawili wilayani Tarime mkoani Mara kufariki dunia kwa nyakati tofauti akiwemo msichana mkazi wa Mtaa wa Nkende, Elizabeth Magige (14) aliyejinyonga kwa kamba kwa madai ya kuzuiliwa na bibi yake kwenda kwenye sherehe za Mwaka Mpya.

Aidha, mkazi wa Kijiji cha Kembwi, Kata ya Manga Tarafa ya Inano, Mariba Nyaronyo (59) amefariki duniani kwa kunywa pombe haramu ya gongo kupita kiasi.

 Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya na madiwani wa kata hizo mbili, walithibitisha vifo vya wananchi wao hao kwa sababu hizo tajwa.

Diwani wa Kata ya Nkende, Daniel Komote alisema “Tukio la msichana Elizabeth Mwita Magige wa miaka 14 kujinyonga nyumbani kwao lilitokea usiku wa kuamkia Januari mosi mwaka huu ambapo kulikuwa na sherehe za disko mjini Tarime ya kuamkia mkesha wa Mwaka Mpya na kuzuiliwa kwenda kuhudhuria mkesha huo. 

“Kitendo kilichomfanya binti huyo kushikwa na hasira na hatimaye kujitia kitanzi na mwili wake kukutwa asubuhi ukiwa unaning’inia ndani ya nyumba jirani na kwa bibi yake huyo aliyemkataza kwenda disko.”

Diwani wa Kata ya Manga, Stephen Gibai alisema, “Mariba Sasi alikuwa mnywaji pombe kali aina ya gongo ambapo ilidaiwa na watu walio karibu naye marafiki zake, siku ya mkesha wa Mwaka Mpya alikunywa pombe nyingi kupita kiasi aina ya gongo kusherehekea mwaka mpya ambayo pombe hiyo ilimdhuru na kufariki dunia.”

Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alithibitisha vifo hivyo viwili.

Samson Chacha  - Habarileo Tarime 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post