POLISI WAKANUSHA TAARIFA YA MAJAMBAZI KUVAMIA GESTI NA KUBAKA WAHUDUMU MBEYA


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linapinga vikali taarifa iliyotolewa na gazeti la Nipashe katika toleo Na.0579824 la Januari 26, 2019 yenye kichwa cha habari “Unyama wa kutisha” Majambazi wavamia gesti, wabaka wahudumu na kupora fedha….baada ya kuwapa vinywaji na biskuti zenye….

Ni kwamba Januari 24, 2019 saa 06.00 asubuhi iliripotiwa taarifa kuwa huko katika Bar na nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Malema iliyopo maeneo ya Makunguru, Kata ya Manga, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya watu watatu waliofahamika kwa majina ya LUCY MWAPASI [36] Mhudumu na mkazi wa Mwanjelwa, CHRISTINA KIPESI [37] Mkazi wa Ituha na DICKSON ALLY [22] Mlinzi na Mkazi wa Makunguru waligundua kuibiwa simu zao za mkononi tano [05] na fedha taslimu za mauzo ya Bar na nyumba ya kulala wageni kiasi cha shilingi 701,000/= na watu wawili wanaowafahamu kwa sura.

Inadaiwa kuwa watu hao walifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni na mmoja wapo alichukua chumba namba 11 ambapo aliishi hapo kwa siku tatu [03] hivyo kujenga mazoea ya karibu na wahudumu hao.

Januari 23, 2019 saa 23:30 usiku muda wa kufunga Bar ulipofika, walibaki wahudumu wawili huku mmoja akiwa wa Bar na mwingine wa nyumba ya kulala wageni na mlinzi ndipo watu hao walitoka chumbani kwao na kuwaambia wale wahudumu kuwa wanataka kuwapa offer ndipo walikubali na kuwanunulia juice ya azam na biskuti wahudumu hao, vitu ambavyo vinadaiwa kuwa na madawa yadhaniwayo ya kulevya na baada ya kula wote walianza kulegea na kulala na kupoteza fahamu na kisha watu hao kutekeleza adhima yao ya wizi.

Wahanga walipata msaada toka kwa wasamaria wema majira ya saa 09:00 asubuhi ambapo walipelekwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu. Kwa mujibu wa mganga wa zamu aliyewafanyia uchunguzi na kugundua kuwa wahanga hao watakuwa wamekula/kunywa chakula chenye sumu au kinywaji chenye sumu hivyo aliwapatia matibabu kuondoa sumu mwilini na baada ya siku moja waliruhusiwa kutoka Hospitalini baada ya kupata nafuu.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya upelelezi wa shauri hili na kubaini kuwa wahudumu hao hawakubakwa kama ilivyoripotiwa katika gazeti tajwa hapo juu. Aidha uchunguzi wa kitabibu uliofanywa na daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya unaonyesha kuwa wahanga wa tukio hili hawakubakwa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linapinga vikali taarifa hiyo iliyotolewa na gazeti la Nipashe na kulitaka gazeti hilo kuomba radhi na kukanusha kupitia gazeti hilo taarifa waliyochapisha kwenye toleo Na. 0579824 la Januari 26, 2019 kwani ni kinyume na kifungu cha sheria ya “Media Service Act 36 (12) ya mwaka 2016 na kifungu cha sheria ya Media Service Act 50 (12) (1) (a) – (f) na (2) (a) – (c) ya mwaka 2016.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527