BOSI FEKI NECTA ASHTUKIWA AKIENDESHA UKAGUZI SHULENI

 
Akiwa ofisini kwake Januari 24 saa nne asubuhi, ofisa Elimu Taaluma Sekondari Mkoa wa Mara, Elisenguo Mshiu alipokea barua kutoka kwa katibu muhtasi wake iliyogongwa muhuri wenye maneno yaliyoandikwa ‘siri’.

Katibu muhtasi alimwambia mleta barua yupo nje na inatakiwa itekelezwe kwa kuwa ilielekezwa kwa ofisa elimu mkoa ambaye alikuwa nje ya ofisi kikazi. Baada ya kuipokea barua hiyo Mshiu alimpigia simu ofisa elimu mkoa kuruhusiwa kuisoma kwa ajili ya utekelezaji.

Ndani ilimtambulisha mleta barua kama naibu katibu mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Salum Athuman na anatakiwa kwenda wilayani Serengeti siku hiyo ili Januari 25 afanye ukaguzi sekondari za Serengeti Nuru na Twibhoki.

Barua hiyo ilisema ukaguzi wake ulilenga kujua kwa nini wanafunzi wa Sekondari ya Serengeti Nuru katika mtihani wa kidato cha nne 2018 wengi wamepata daraja sifuri na Twibhoki kuna walimu wengi kutoka Kenya. Hata hivyo, licha ya Mshiu kudai kuwa naibu katibu mkuu Necta aliyetajwa anamfahamu kwa sura kwa kuwa aliwahi kufanya naye kazi, hakuweza kushtuka baada ya kukutana na sura tofauti na anayoifahamu.Bosi abanwa

Mleta barua alimbana Mshiu waondoke bila kupita popote hadi Serengeti akiahidi kuwa fedha za kujikimu njiani atampata.

Katika kuonyesha kubana matumizi, bosi huyo feki alimtaka ofisa elimu wapande bajaji kutoka mjini Musoma hadi stendi ya Bweri, na akamtaka alipe Sh3,000.

Vilevile, Mshiu aliagizwa kulipa nauli ya watu wawili ya Sh12,000 (yeye na mtu huyo) kutoka Musoma hadi Mugumu, Serengeti na baada ya kufika akatakiwa kulipia gharama za vyumba vya kulala.

Bosi huyo feki alimtaka watafute vyumba vya Sh10,000 kama njia ya kubana matumizi.

“Tulipofika Nyumba ya Kulala (Wageni ya) Buruna nililazimika kulipia vyumba viwili kila kimoja Sh15,000, (yeye) akawa namba saba mimi sita,” alisema Mshiu.

“Chakula niliona mfukoni hali mbaya, nikaagiza ugali mbogamboga na maziwa yeye akaagiza wali kuku, nikalipia.”

Vilevile, ‘bosi huyo’ aliagiza amtaarifu ofisa elimu sekondari wilayani humo, William Makunja juu ya uwepo wake na kazi iliyowapeleka. “Nilitoa taarifa na Januari 25 tulifika ofisini na kumkuta (Makunja) akijiandaa kwenda Musoma na kutukabidhi ofisa elimu sekondari taaluma, Enock Ntaksigaye akatupeleka kwa gari Nuru Sekondari.”

Aanza ‘ukaguzi’

Mkuu wa shule hiyo, Benjamin Ng’oina alisema alitaarifiwa na ofisi ya elimu sekondari Januari 24 jioni kuhusiana na ukaguzi na baada ya kukutana na ‘bosi huyo wa Necta’ alimpa ushirikiano.

Alisema baada ya kufika shuleni hapo, aliomba kufuli ili aifunge shule hiyo kwa madai kuwa walimu walichelewa kufika.

Mtu huyo alianza ‘ukaguzi’, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda walianza kumshtukia. “Kwanza barua yake inadai anakuja kukagua shule yetu kwa nini wanafunzi wamepata daraja sifuri, nilikataa kwa kuwa walisajiliwa wanafunzi 55, waliofanya ni 51, daraja la kwanza mmoja, la pili 10, la tatu 23 na daraja la nne 17, hakuna ziro. Nilianza kupata wasiwasi,” alisema Ng’oina.

Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post