MAHAKAMA YAAMURU KUFUKULIWA KWA MWILI ULIOZIKWA MWAKA JANA


Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, imeamuru kufukuliwa kwa mwili wa marehemu Benedict Msote (68), aliyefariki dunia miezi minne iliyopita ili ufanyiwe uchunguzi wa chanzo cha kifo chake.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kuwepo ubishani kati ya taarifa zilizoandikwa na Mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kuhusu chanzo cha kifo cha Msote aliyefariki dunia Oktoba 5, 2018.

Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa Pascal Mayumba, aliamua kutoa kibali hicho kutokana na kuwepo kwa taarifa za kuchanganya kuhusu chanzo kifo cha marehemu huyo.

Aidha Hakimu Mayumba ameiambia mahakama hiyo kwamba polisi wilayani hapa walitoa ombi la kufukuliwa mwili wa Msote baada ya kuwepo kwa malalamiko ya kuwa kifo chake kilitokana na kipigo na si shinikizo la damu kama inavyodaiwa.

 Ofisa Upelelezi wa Polisi Mjini Mpwapwa, Makubura Kati alisema, ndugu wa marehemu walipeleka malalamiko kuwa kifo cha ndugu yao kilitokana na kipigo.

Pia ulizikwa kabla mwili huo haujafanyiwa uchunguzi. Hadi sasa kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Emanuel Sindato amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kusababisha kifo hicho.

 Mmoja wa watoto wa marehemu, Julius Msote alisema waliamua kufukua mwili wa baba yao baada ya kubaini kuwa kifo chake hakikutokana na shinikizo la damu kitu alichokisema kilitokana na kipigo.

“Mwili wa baba tangu unafikishwa hospitalini ulitokana na kipigo na hata Fomu ya Polisi namba tatu (PF3) tulijaza, sasa ninashangazwa kuambiwa mzee alifariki dunia kwa shinikizo la damu, tatizo ambalo hajawahi kuwa nalo katika maisha yake yote,” alisema.

Aidha alisema wanasubiri taarifa ya daktari aliyefanya uchunguzi huo na kubaini chanzo cha kifo cha baba yao. 

Uchunguzi huo ulifanywa na Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya, Dk Hamza Mkingule na Bibi Afya wa Wilaya, Merry Mabangwa chini ya uangalizi wa Polisi wa Kituo Kikuu cha Wilaya. 

Uchunguzi huo uliofanywa na Mganga Mfawidhi na watendaji wengine utawasilishwa Januari 25,kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post