HUYU NDIYE FELIX TSHISEKEDI MSHINDI WA URAIS CONGO

Felix Tshisekedi akiwa katika mkutano wa kisiasa Aprili 2018 mjini Kinshasa
***
Felix Tshisekedi Tshilombo, ni mwanawe mwanzilishi wa chama cha UDPS, mwanasiasa wa upinzani wa muda mrefu Etienne Tshisekedi.

Babake alifariki Februari mwaka jana na sasa mwanawe anatarajia kutumia msingi wa umaarufu wa babake kuchaguliwa kuwa rais.

Marafiki zake humuita kwa jina la utani "Fatshi" kutokana na hali kwamba yeye ni mnene kiasi, na pia ni ufupisho wa jina lake Fe (lix) Tshi (lombo).

Kwa muda ilionekana kana kwamba Tshishekedi, 55, jina lake halingekuwa kwenye karatasi za kura.

Novemba 11, yeye na Vital Kamerhe pamoja na wagombea wengine watano wa vyama vya upinzani walikutana na kumchagua Martin Fayulu apambane na Emmanuel Ramazani Shadary.

Lakini makubaliano yao yalidumu saa 24 pekee.

Tshisekedi na Kamerhe walidai kushinikizwa na vyama vyao kujiondoa na wakajitenga na Fayulu hatua iliyougawanya upinzani.

Wakishinda, Tshisekedi atakuwa rais naye Kamerhe, ambaye ni rais wa zamani wa Bunge na ambaye aliwania dhidi ya Kabila mwaka 2011 awe waziri mkuu.

Tangu babake Tshisekedi alipoanzisha chama cha UDPS mwaka 1982, kilihudumu kama chama kikuu cha upinzani, mwanzoni wakati wa utawala wa Mobutu Sese Seko kisha wakati wa utawala wa babake Kabila, Laurent-Desire Kabila, aliyeongoza 1997 hadi kifo chake 2001.

Kujiondoa kwa Tshisekedi kutoka kumuunga mkono Fayulu kulizua lawama, kwani kuliugawanya upinzani uliokuwa umeonesha dalili za kuungana.

Tshisekedi ni baba wa watoto watatu na yeye na Fayulu ni waumini katika kanisa moja la kipentekoste jijini Kinshasa.

Watakuwa wanawania dhidi ya Shadary ambaye ni Mkatoliki.

Tshisekedi ana stashahada katika mauzo na mawasiliano kutoka Ubelgiji, lakini wakosoaji wake hutilia shaka hilo.

Wakosoaji wake pia wamekuwa wakisema hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa juu au kuwa na uzoefu wa usimamizi.

Lakini amepanda cheo chamani, kuanzia mwaka 2008 ambapo alikuwa katibu wa taifa aliyeangazia masuala ya uhusiano wa nje.

Machi mwaka jana aliteuliwa kiongozi wa chama baada ya kifo cha babake.
Alichaguliwa kuwa mbunge 2011, akiwakilisha eneo la Mbuji-Mayi katika mkoa wa Kasai-Oriental lakini alikataa kuhudumu kwa kuwa hakutambua kushindwa kwa babake na Rais Kabila katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2011.

Tshisekedi, ingawa hana uungwaji mkono mkubwa kama wa babake, aliambia AFP mwaka jana kwamba akishinda urais ataunda tume ya ukweli, haki na maridhiano na kumuwajibisha Bw Kabila. Lakini alisema atamruhusu kusalia nchini DR Congo.

Walioruhusiwa kuwania urais DR Congo

 • Emmanuel Ramazani Shadary
 • Kikuni Masudi Seth
 • Mukona Kumbe Kumbe Pierre
 • Ngoy Ilunga Isidore
 • Makuta Joseph
 • Kabamba Noel
 • Mabaya
 • Kinkiey Mulumba
 • Freddy Matungulu
 • Felix Tshisekedi
 • Allain Shekomba
 • Radjabu Sombolabo
 • Kamerhe Vital
 • Fayulu Martin
 • Bomba
 • Gabriel Mokia
 • Basheke Sylvain
 • Charles Gamena
 • Mbemba Francis

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post