WANAJESHI WATANGAZA KUMPINDUA RAIS BONGO

Kundi la maofisa wa jeshi nchini Gabon limetangaza kwamba limetekeleza mapinduzi ya serikali katika taifa hilo la Afrika Magharibi iliyokuwa ikiongozwa na Rais Ali Bongo.

Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vimesema kwamba taarifa ya wanajeshi hao kufanya mapinduzi imetangazwa katika kituo cha redio cha serikali majira ya saa kumi na mbili alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki.

Imeelezwa kwamba wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita yanaendelea na doria katika barabara za mji mkuu Libreville. Shirika la habari la AFP inasema milio ya risasi imesikika jijini humo.

Wanajeshi hao wamesema wamechukua hatua hiyo "kurejesha demokrasia" na wametangaza kwamba wanataka kuunda 'Baraza la Taifa la Ufufuzi/Ukombozi' huku wakikosoa hotuba ya Mwaka Mpya iliyotolewa na Rais Bongo mnamo 31 Desemba.

Mapinduzi hayo yamefanywa wakati Rais Bongo akiwa nje ya nchi hiyo kwa zaidi ya miezi miwili, akipokea matibabu nchini Morocco kutokana na maradhi ambayo hayajafichuliwa baada ya kuugua akiwa ziarani Saudi Arabia, 24 Oktoba.

Rais Ali Bongo alianza kuiongoza Gabon 2009 kwa mara ya kwanza na baadaye katika uchaguzi wa marudio uliofanyika 2016 ambapo inaelezwa kuwa alipokea madaraka kutoka kwa baba yake Omar Bongo ambaye aliiiongoza nchi hiyo ya Afrika magharibi kwa zaidi ya miaka 40.

Chanzo:Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post