Picha : MIGODI YA BUZWAGI , BULYANHULU YATOA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI WA SHULE KAHAMA


Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Acacia kupitia migodi yake ya Buzwagi na Bulyanhulu imetoa msaada wa mabati 2347 yenye thamani ya shilingi milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu katika shule za msingi na sekondari kwenye halmashauri za wilaya ya Msalala na Kahama Mji mkoani Shinyanga. 



Mabati hayo yenye geji 28  yamekabidhiwa leo Januari 16,2019 kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha na Meneja Mwendeshaji mgodi wa Buzwagi, Arthur Mgongo akimwakilisha Meneja mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu. 



Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mgongo alisema Acacia inaunga juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025. 



"Katika muitikio wa ombi la msaada wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya madarasa na nyumba za walimu,migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu imechangia vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 150,mpaka sasa tumechangia mifuko ya saruji 3200 ambapo halmashauri ya Kahama Mji imepokea mifuko 1600 ya saruji na Msalala mifuko 1600 jumla ina thamani ya shilingi milioni 80",alieleza Mgongo.  

"Kiasi cha ziada ya fedha iliyobaki ambacho ni sh. Milioni 70 kimetumika kununua mabati haya 2347 yaani mabati 1173 kwa Halmashauri ya Kahama Mji na mabati 1174 Msalala",aliongeza Mgongo. 

Alisema msaada huo utasaidia kuongeza miundo mbinu katika shule ili kukidhi ongezeko la wanafunzi kwani tangu serikali ianze utekelezaji wa mpango wa kutoa elimu bure,uandikishaji wa wanafunzi shuleni umeongezeka na uhitaji wa miundombinu umeongezeka. 

Mgongo alielezea kuwa, kupitia mpango wake wa maendeleo ya jamii, Acacia imeendelea kuboresha upatikanaji wa elimu katika jamii zinazozunguka migodi yake na kuleta mapinduzi ya kijamii na kiuchumi nchini sambamba na ajenda kuu ya viwanda. 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha aliishukuru Acacia kwa kuwa sehemu ya jamii kuchangia sekta ya elimu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Macha alisema wilaya yake ina uhitaji wa madarasa 250 na kubainisha kuwa mabati yaliyotolewa na Acacia yatatumika kwenye ujenzi wa madarasa 50 huku akitaja kipaumbele ni kwenye shule ambazo tayari wazazi wamejenga maboma. 

Aidha aliwataka wadau kushirikiana na serikali kuchangia kwenye elimu kwani kila mmoja ni sehemu ya jamii hivyo anatakiwa kuchangia badala ya kuiachia serikali pekee.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI

Mwendeshaji mgodi wa Buzwagi, Arthur Mgongo akizungumza kwa niaba ya Meneja mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu wakati akikabidhi mabati  2347 yaliyotolewa na Acacia kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya Kahama Mji na Msalala leo katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kahama.Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog


Mgongo akishikana mkono na Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha (kulia) wakati akikabidhi mabati  2347 (pichani nyuma) yaliyotolewa na Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya Kahama Mji na Msalala. Kulia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama Mji, Abel Shija.

Mgongo akielezea shughuli zinazofanywa na Acacia katika jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maktaba mjini Kahama,Nyang'hwale na Tarime lakini pia maboresho na utanuzi wa shule za msingi na sekondari ikiwemo ujenzi wa maabara na mabweni. Acacia pia inadhamini wanafunzi  wanaoishi katika mazingira magumu kupitia programu ya CanEducate.
Awali Mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama Mji, Anderson Msumba akiangalia mabati matatu kati ya 2347 ambapo 1173 ni kwa ajili ya Kahama Mji yaliyotolewa na migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu.
Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha akizungumza wakati akipokea mabati yaliyotolewa na Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia kupitia migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu.
Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akiishukuru Acacia kwa kuendelea kuwa mdau muhimu wilayani Kahama kwa kuchangia shughuli za maendeleo.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kahama Mji, Abel Shija akielezea jinsi Acacia wanavyoshirikiana na halmashauri hiyo kuwaletea maendeleo wananchi.


Katibu wa CCM wilaya ya Kahama Alexandrina Katabi (kwanza kushoto) akizungumza wakati wa makabidhiano ya mabati ambapo alisema mchango wa Acacia ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
Viongozi mbalimbali wa halmashauri  ya wilaya ya Kahama Mji na Msalala na waandishi wa habari wakiwa katika hafla fupi ya makabidhiano ya mabati.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527