TSUNAMI YAUA WATU ZAIDI YA 160 INDONESIA


Watu 168 mpaka sasa wameripotiwa kupoteza maisha huku 750 wakijeruhiwa vibaya nchini Indonesia baada ya Tsunami kuikumba nchi hiyo siku ya jana usiku.

Mamlaka nchini humo zinasema Tsunami hiyo imetokea katika fukwe za visiwa vya Java na imesababishwa na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mlipuko wa volkano.


Msemaji wa Taasisi inayoshughulika na kuzuia majanga nchini humo, Sutopo Purwo Nugroho amesema mpaka sasa watu 30 hawajulikani walipo, huku nyumba 558, migahawa 60 ikibomolewa na Tsunami.

Nugroho amesema tukio hilo ni la kushtukiza, kwani hakukuwa na taarifa wala tahadhari yoyote ile iliyotolewa kwa wananchi.

Usiku wa Jumamosi siku ya tukio, Bendi ya muziki maarufu nchini humo ya Band Seventeen, ikiongozwa na msanii wa muziki, Riefian Fajarsyah nayo ilipatwa na kazia baada ya jukwaa lao kufunikwa na maji.


Kupitia ukurasa wa Instagram wa Riefian Fajarsyah amethibitisha kuwa watu wanne kutoka kwenye bendi yake wamefariki dunia.


Mwezi kama huu mwaka 2004, tsunami kama hiyo ilitokea katika bahari ya Hindi kufuatia tetemeko la ardhi, iliua zaidi ya watu 226,000 katika nchi 13 ikiwa 120,000 walikufa nchini Indonesia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527