RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MAKAMU MKUU WA UDOM PROF. EGID BEATUS MUBOFU

Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Benjamin Mkapa kufuatia kifo cha Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Egid Mubofu.

Profesa Mubofu amefariki dunia leo Jumanne Desemba 18, 2018 Pretoria, Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu zaidi akitokea taasisi ya tiba ya mifupa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Moi) alikokuwa akipatiwa matibabu ya kiharusi.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inasema Rais Magufuli amemuomba Mkapa kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya marehemu, wahadhiri, wanafunzi na wafanyakazi wa Udom na kwenye jumuiya na taasisi zote ambazo marehemu alifanya kazi.

“Nimesikitishwa sana na kifo cha Profesa Mubofu, nitamkumbuka kwa uchapakazi wake, ubinifu, uadilifu na uaminifu mkubwa aliouonesha katika utumishi wake kwa Taifa ikiwemo kazi nzuri aliyoifanya katika Shirika la Viwango la Taifa (TBS) akiwa mkurugenzi mkuu kabla ya kuteuliwa kuwa makamu mkuu wa Udom,” amesema Rais Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post