NDEGE MPYA MBILI AIRBUS 220-300 KUINGIA NCHINI MUDA WOWOTE

Ndege mbili mpya aina ya Airbus 220-300 zilizotegemea kuwasili nchini Desemba mwaka huu, moja imeshakamilika na kufanyiwa majaribio ya kuruka, ambayo yameleta matokeo mazuri.

Kinachosubiriwa sasa ni timu ya makabidhiano kutoka Tanzania kufika Canada kwa ajili ya kuzipokea na kuzileta. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Ladslaus Matindi alisema siku chache zilizopita ndege moja kati ya hizo mbili, ilifanya majaribio ya kuruka na kuleta matokea mazuri, hivyo kinachosubiriwa ni timu ya makabidhiano kuwasili nchini humo.

“Ndege mpya mbili tunazotarajia kuzipokea hivi karibuni, moja tumepata maendeleo yake imefanyiwa majaribio ya kuruka juzi na matokeo ni mazuri sana, timu ya wataalamu wetu inaondoka wiki ijayo kwenda Canada kwa ajili ya makabidhiano na kuzileta,”alisema Matindi.

Aliongeza, ndege ya pili nayo iko kwenye hatua za mwisho za uundwaji na iko vizuri na kwamba timu ya wataalamu kutoka Tanzania, ilishawasili nchini humo kwa ajili ua ukaguzi na kutoa ripoti yao ya maendeleo ya ndege hizo.

Matindi alisema baada ya ndege ya kwanza kuwa tayari, timu hiyo wataalamu na makabidhiano, itasubiri ndege ya pili ifanyiwe majaribio, kisha kuangalia vitu vyote kama viko sawa na hatua ya mwisho ni kuzisafirisha kuja nchini.

Akizungumzia ndege hizo, ambazo awali zilipaswa kuwa tayari na kuwasili nchini Novemba mwaka huu, Matindi alisema walipokea maombi kutoka kwa watengenezaji wa ndege hizo, kampuni ya Airbus nchini Canada ya kusogeza mbele tarehe ya kuzikabidhi ili kumalizia mambo madogo ya matengenezo yaliyosalia.

“Ni kweli awali tulikuwa tuzipokee ndege hizo Novemba mwaka huu, lakini watengenezaji wametuomba na ni kitu cha kawaida, kusogeza mbele muda wa kuzikabidhi ili tuzipokee wakati wowote kuanzia sasa,”alisema Matindi.

Ndege hizo mbili kila moja ina uwezo wa kubeba abiria 132, ambapo daraja la kwanza ni abiria 12 na daraja la kawaida ni abiria 120. 

Awali, ndege hizo zilijulikana kwa jina la Bombardier C Series, na Julai mwaka huu kampuni ya Airbus iliingia mkataba wa ununuzi na kuzibadilisha jina na kuziita A220-100/300 .

tazama hapa chini ndege mpya ikifanyiwa majaribio
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post