BASATA YAKANUSHA KUWAFUNGULIA DIAMOND NA RAYVANNY

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) nchini Tanzania limekanusha kuwafungulia wasanii Diamond Platnumz na Rayvanny wanaotumikia adhabu ya kutojihusisha na sanaa kwa muda usiojulikana baada ya kufanya makosa mbalimbali ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Taarifa ya Naibu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Onesmo Kayanda iliyotolewa leo Jumamosi Desemba 22, 2018 imesema haijawaondolea adhabu hiyo na kuwakata wafuate maagizo waliyopewa ikiwamo kutofanya maonyesho nje ya nchi.

Jana, wasanii hao kupitia mtandao wa Instagram waliomba radhi kwa mamlaka mbalimbali nchini na jioni walionekana wakifanya mkutano na wanahabari nchini Kenya kutangaza maonyesho yao yanayoendelea.

"Ikumbukwe kuwa Desemba 18 tuliwafungia kutojihusisha na sanaa kwa kipindi kisichojulikana kwa kuimba kwa makusudi wimbo Mwanza tulioufungia kwa sababu za kimaadili,

"Baraza linasisitiza kuwa halijawafungulia wasanii hao, pia linawaonya kuacha kutoa taarifa za uongo kabla halijawachukulia hatua kali zaidi," imesema taarifa hiyo ya Kayanda.

Diamond na Rayvanny wameingia matatani wakituhumiwa kufanya makosa mbalimbali ikiwamo la kutumbuiza wimbo uliofungiwa, kufanya tamasha mkoani Mwanza bila kibali, kutoa lugha ya matusi jukwaani mkoani Mtwara na kutofuata taratibu za usajili wa matamasha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527