MKUU WA MAJESHI AOMBA VIONGOZI WA DINI KUDUMISHA AMANI..ASKOFU SANGU ANENA

Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini Jenerali Venance Mabeyo ametoa wito kwa Viongozi wa Dini nchini kuendelea kuhubiri amani ili kujenga jamii iliyo bora yenye kudumisha upendo na mshikamano.

Jenerali Mabeyo ametoa wito huo wakati wa ibada ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro, Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwepo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Benard Kibese na viongozi wengine wa Chama na Serikali, ambapo alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo kwa Taifa lolote duniani.

“Suala la amani na utulivu ni la msingi sana katika nchi yetu, kwa vile kila mwananchi ana dini yake tunaamini kuwa viongozi wa dini zote kwa kuwa wanasikilizwa sana na waumini wakiweka msisitizo katika suala la amani, amani itatawala na kutakuwa na utulivu”

“Utulivu huu tunauhitaji sana ili tupate maendeleo, kama viongozi wetu wa kisiasa wanavyosisitiza kuwa tudumishe amani na utulivu tupate maendeleo, bila utulivu watu wakiwa wanahaingaika hakuna maendeleo kwa sababu hakuna shughuli mtu anaweza kufanya kama hana amani na utulivu, hivyo hataweza pia kuleta maendeleo yake, familia, jamii na Taifa kwa ujumla” alisema Jenerali Mabeyo

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Simon Sirro amesema vitendo vingi vya uvunjifu wa amani na uhalifu ikiwemo ukataji wa mapanga na mauaji ya vikongwe na yanachangiwa na watu kukosa hofu ya Mungu; hivyo nyumba za ibada(makanisa na misikiti) zinapojengwa kwa wingi zitakuwa msaada mkubwa sana kwa watu kuwa na hofu ya Mungu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema jamii inayoamini uwepo wa Mungu haiwezi kuwa na vitendo vya kisasi, kukatana mapanga na mauaji ya vikongwe huku akiwaasa Watanzania kukaa kwa amani na upendo bila kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha amani.

Akibariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro, Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega, Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Muhashamu Liberatus Sangu amewataka Watanzania kupendana na kuacha roho ya ubinafsi na visasi.

Aidha, Askofu Sangu ametoa wito kwa viongozi na waumini kufanya nyumba za ibada zibaki nyumba za sala kama yanenavyo maandiko matakatifu na kamwe zisitumike kama majukwaa la wanasiasa.

” Palipo na msamaha pana umoja, uelewano na usawa lakini palipo na kisasi hapana maendeleo; nyumba ya ibada isitumike kama jukwaa la Wanasiasa alisisitiza Muhashamu Askofu Sangu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527