YANGA YAENDELEZA KUWEKA REKODI ZAKE VIZURI


Wachezaji wa Yanga wakifurahia ushindi

Klabu ya Yanga imeendeleza rekodi yake nzuri dhidi ya Kagera Sugar katika uwanja wa Kaitaba kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mfululizo wa mechi za ligi kuu Tanzania bara TPL.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo yameyofungwa na Heritier Makambo katika dakika ya 21 na Raphael Daudi katika dakika ya 75 huku bao pekee la Kagera Sugar likifungwa na Ramadhan Kapera katika dakika ya 32 ya mchezo.

Ushindi huo wa Yanga dhidi ya Kagera Sugar hii leo, unaifanya klabu hiyo kukusanya alama sita katika michezo yake miwili tangu ilipoanza kucheza mechi zake za ligi kuu nje ya uwanja wa taifa, baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Mwadui Fc katikati ya wiki.

Yanga inafikisha alama 32 nyuma ya alama moja pekee dhidi ya vinara Azam Fc ambayo ina alama 33 baada ya kushuka dimbani michezo 13 huku Yanga yenyewe ikiwa imeshacheza michezo 12. Nafasi ya tatu inashikiliwa na Simba yenye alama 27.

Yanga inazidi kudhihirisha ubora wake katika michezo ya ligi kuu msimu huu, ikiwa haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa sawa na Azam Fc.

Ikidhihirisha pia kuwa haifungiki katika mechi za ugenini tofauti na mpinzani wake Simba ambayo inapata changamoto hasa katika mechi za ugenini ikiwa tayari imefungwa mechi moja na Mbao Fc katika uwanja wa CCM Kirumba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527