RAIS MAGUFULI AMTUMA LOWASSA AWAAMBIE WAPINZANI WENZAKE WATULIE…LA SIVYO WATAISHIA GEREZANI

Rais wa Tanzania, John Magufuli amemwambia waziri mkuu wa zamani, Edward Lowasa awaambie viongozi wengine wa upinzani watulie “la sivyo wataishia gerezani”.

Rais alisema hayo baada ya kumsifu Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, kuwa ni mwanasiasa mstaarabu ambaye alionyesha utulivu hata baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.

Alisema hayo katika uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo Jumanne (Novemba 27) uliohudhuriwa na Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

"Ninakupongeza sana (Lowassa). Hii ndiyo Tanzania mpya tunayoitaka. Vyama vyetu visiwe chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo," amesema Magufuli.

"Nimezungumza hili kwa heshima kubwa ili ukawashauri wale unaowaongoza watulie vinginevyo wataishia kwenye magereza."

Hadi sasa, viongozi kadhaa wa upinzani, hasa Chadema waka kesi za aina tofauti katika mahakama mbalimbali nchini; baadhi wakishtakiwa kwa uchochezi, wengine kwa kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais na wengine kwa kufanya mikusanyiko bila ya kibali.

Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifutiwa dhamana pamoja na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria.

Lakini Lowassa, ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu kujivua uanachama wa CCM na kujiunga na upinzani, hajawahi kukumbwa na matatizo dhidi ya mamlaka, zaidi ya kuitwa kituo cha polisi kutoa maelezo.

Lowassa alihamia upinzani mwaka 2015 akipinga kitendo cha Kamati Kuu ya CCM kuondoa jina lake na la wagombea wengine wa urais na kujiunga na Chadema, ambayo ilimpa fursa ya kutimiza ndoto yake ya kugombea urais.

Katika harakati zake, Lowassa aliungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioundwa na Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi na kushika nafasi ya pili, akiwa ameweka rekodi ya upinzani kupata kura nyingi. Alipata kura milioni 6.7, akiwa nyuma kidogo ya Rais Magufuli, aliyepata kura milioni 8.8.

Akizindua maktaba hiyo ya kisasa yenye uwezo wakuchukua wanafunzi 2,100 na kutunza vitabu 800,000, Rais Magufuli amesema heshima iliyojengwa na UDSM inatakiwa iendelee kuwepo na wanafunzi wapate yanayostahili kwa wakati.
Via >>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527