Picha : MWANASOKA MAARUFU SUDI DAGHESHI AZIKWA MJINI SHINYANGA


Sudi Dagheshi (45) mkazi wa mjini Shinyanga, ambaye alikuwa mchezaji wa timu ya Pamba, Igembe Nsabo,Veterani, Polisi Shinyanga na kocha wa timu ya Mwadui Fc ilipokuwa daraja la kwanza na kuipaisha kucheza msimu wa ligi kuu bara, amefariki ghafla na kuzikwa kwenye makaburi ya waislamu Nguzo Nane mjini Shinyanga.


Aidha mazishi ya mwanasoka huyo yameongozwa na Shekhe wa mkoa wa Shinyanga Ismail Makusanya.

Marehemu Dhagheshi alifariki usiku wa kuamkia Jumatano Novemba 7,2018 majira ya saa sita usiku katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kuugua ghafla na kukimbizwa kupatiwa matatibu, ambapo madaktari walijaribu kuokoa uhai wake lakini ilishindikana na akafariki dunia.

Akisimulia  kuhusu kifo cha mwanasoka huyo leo Novemba 8,2018, mtu wa karibu na familia Salumu Kitumbo, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Shinyanga (SHIDIFA), alisema marehemu alifariki kwa ugonjwa wa kisukari pamoja na Shinikizo la damu.

Alisema siku ya Oktoba 28 mwaka huu walipotoka kucheza Dodoma soka la wakongwe (Veterani), marehemu alikuwa analalamika anajisikia vibaya, lakini muda kidogo akapata nafuu akaendelea na shughuli zake, ambapo juzi akapata taarifa kuwa ameugua ghafla na ndipo wakamkimbiza hospitali na kufariki dunia.

“Marehemu ameacha pengo kubwa sana kwa wadau wa soka mkoani Shinyanga, kwani alikuwa mtu wa michezo muda wote na alikuwa akijitolea sana kuibua vipaji vya vijana, na ndiye aliyeipaisha Timu ya Mwadui Fc kuanza kushiriki kucheza msimu wa Ligi kuu bara,”alisema Kitumbo.

“Mbali na ukocha marehemu pia aliwahi kuchezea Timu ya Pamba, Igembe Nsabo, Polisi Shinyanga, pamoja na Vetereni timu ya wakongwe, ambayo alikuwa akiendelea kuichezea hadi mauti inamfika,”aliongeza.

Naye mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu mkoani Shinyanga Benista Lugola, alisema kifo cha mwanasoka huyo ni pigo kwa mkoa huo, ambaye alikuwa akichagua wachezaji bora wa ligi kuu Man of the match kwenye kituo cha Mwadui,

Kwa upande wake mtoto wa marehemu Mohamedi Sudi, alisema marehemu baba yake ameacha mjane pamoja na watoto wanne.


TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI


Shekhe wa mkoa wa Shinyanga Ismail Makusanya akiongoza mazishi wa mwanasoka Sudi Dagheshi kabla ya kwenda kumpumzisha kwenye makazi yake ya milele.


Marehemu Sudi Dagheshi enzi wa uhai wake.

Awali mwili wa marehemu Sudi Dagheshi ukitolewa ndani ya nyumba yake kwa ajili ya maandalizi ya kwenda kumpumzisha kwenye makazi yake ya milele.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Shinyanga Salumu Kitumbo, ambaye pia alikuwa rafiki mkubwa wa marehemu Sudi Dagheshi akizungumza na waandishi wa habari jinsi  umauti ulivyomkuta mwanasoka huyo na alivyoacha pengo kwa wadau wa michezo mkoani Shinyanga.

Wadua wa michezo wakiwa nyumbani kwa marehemu Sudi Dagheshi , kwa ajili ya kwenda kumpumzisha kwenye makazi yake ya milele.

Wadau wa michezo wakiwa kwenye maombolezo ya mwanasoka Sudi Dagheshi aliyefariki ghafla kwa ugonjwa wa Kisukari na Shinikizo la damu.

Mwili wa marehemu Sudi Dagheshi ukipakiwa kwenye gari kwenda kumstiri kwenye makazi yake ya milele.

Mwili wa marehemu Sudi Dagheshi ukiwasili kwenye makaburi ya waislamu eneo la Nguzo Nane kwa ajili ya kuupumzisha kwenye makazi yake ya milele.

Wadau wa michezo wakimpumzisha mwanasoka Sudi Dagheshi kwenye makazi yake ya milele katika makaburi ya waislamu nguzo nane.

Na Marco Maduhu- Malunde1 Blog.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527